●Inadumu zaidi ya masaa matatu
●Rafiki kwa mazingira
●Rafiki wa bei
*Dodoma*
Katika mwendelezo wa kuwahimiza na kuhamasisha watanzania katika kutumia Nishati safi ya Rafiki Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imetumia maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya Rafiki Briquettes.
Akiongea wakati wa kutoa elimu katika banda la STAMICO, Meneja Masoko na Uhusiano Bw. Deus Alex amezungumzia azma ya kuhakikisha kuwa nishati hii inawafikia watu wengi ili kuweza kupunguza matumizi ya Kuni na Mkaa unaotokana na Miti.
Ameongeza pia, katika maonesho hayo STAMICO imeleta bidhaa za kokoto kwa ajili ya Watanzania wanaohitaji kwa ajili ya ujenzi mkubwa na mdogo. Uzalishaji huo wa Kokoto unapatikana eneo la Chigongwe barabara ya Singida.
Akielezea kuhusu nishati hiyo, Deus amefafanua kuwa nishati hii utokana na mabaki ya makaa ya mawe yanayochimbwa katika mgodi wa Kabulo - Kiwira mkoani Songwe ambapo mabaki hayo hupitia mchakato wa kiwandani kupunguza joto na kuondoa hewa zisizo rafiki kwa matumizi ya nyumbani.
Sambamba na mradi huo, Deus ametoa mwaliko kwa wachimbaji wadogo kutembelea maonesho hayo ili waweze kupata elimu na huduma zinaozohusiana na uchimbaji ndani ya mabanda ya Wizara ya Madini.
Kupitia STAMICO, Serikali mpaka sasa imenunua mitambo 15 Kwa ajili ya kuwahudumia wachimbaji wadogo ili kuwaongezea tija katika shughuli za uchimbaji wa Madini nchini.
Aidha, Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Mkoa wa Dodoma amewaita washiriki wote na watanzania kwa ujumla kufika katika kontena lililopo eneo la manispaa ya zamani ya Dodoma, sabasaba ili waweze kujipatia huduma ya Nishati Safi ya Rafiki Briquettes.
Kwa upande wa Taasisi ya Foundation for Disalities Hope Bi. Elizabeth Bundala ametoa rai kwa watanzania wote kutembelea mabanda yaliyo chini ya Wizara ya Madini kujipatia taarifa za mnyororo wa thamani madini.