Na Ada Ouko, Musoma.
WANANCHI takribani 1250 wa kijiji cha Muhoji kata ya Bugwema Halmashauri ya Musoma vijijini wamefanikiwa kuondokana na kero ya kutokupata huduma ya maji safi na salama ambayo walikuwa wakiyatumia kwa kushirikiana na wanyama mbalimbali sambamba na mifugo yao tatizo lililokuwepo takribani miaka 64 ya uhuru nchini.
Changamoto hiyo imetatuliwa baada ya serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira (RUWASA) kuanzisha mradi wa uchimbaji visima na ujenzi wa vioski wilayani humo programu ambayo inatekelezwa katika vijiji vinne vya Muhoji, Masinono, Kiriba na Bugwema.
Akizungumza Agosti 16,2025 mara baada ya kuzindua mradi huo kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ussi alisema jamii ya kijiji cha Muhoji wanayo matumaini makubwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
" Rais Samia Hassan katika adhma yake ya kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo kuboresha miundombinu ya maji safi na salama, kwakweli hakubabaika kwenye hili ambapo alianza kutekeleza baraza la mawaziri na kisha kuunda wizara hii ya maji na ni wizara pekee inayojitegemea ili kuweza kutekeleza jukumu la maji" Alisema Ismail.
Amesema sema baada ya Rais Samia kuunda wizara hiyo aliendelea kwa kusikiliza malalamiko ya wananchi wengi wanaoishi vijijini, mitaani, na katika Kata mbalimbali na aligundua hawana maji safi na salama, kisha akaamua kuunda mamlaka itakayosambaza maji vijijini inayojulikana kwa jina la Ruwasa.
"Nimefarijika kwa sababu nyinyi wenyewe wana Muhoji mmeridhia kuukubali na kuupokea mradi huu wa maji safi na salama ombi langu kwenu mshirikiane kwa pamoja kulinda na kutunza miundombinu hii ya sekta ya maji, Serikali tayari imeshaleta fedha nyingi, na Halmashauri ya Musoma DC ni miongoni mwa jimbo limepewa zaidi ya visima vitano" aliongeza kusema.
Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa wilayani hapa Edward Sironga amesema mradi wa uchimbaji wa visima na ujenzi wa vioski vya maji unatekelezwa nchini kote kwa kila jimbo la uchaguzi vijijini ambapo tayari visima vinne(4) vimechimbwa huku ujenzi wa vioski unaendelea na kwamba mradi huo umefikia asilimia 75 ya utekelezaji wake.
"Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.2 kwa majimbo ya uchaguzi mkoa wa Mara,hivyo kwa jimbo la Musoma vijijini zaidi ya kiasi cha shilingi milioni 208 zitatumika kukamilisha ujenzi wa vioski 5, na zaidi ya shilingi milioni 41 zitatumika kwa kila kiosk"
Amesema miongoni mwa shughuli zinazotekelezwa na mradi huo ni pamoja na ujenzi wa vioski 5, ununuzi wa pampus 5, ununuzi wa solar za 370 watt, ununuzi wa bomba na ununuzi wa matanki ya plastiki ya maji, na kwamba katika kiosk cha kijiji cha Muhoji jumla ya wananchi wapatao 1,200 watapata huduma ya maji safi na salama.
Naye aliyekuwa Diwani wa kata hiyo Clifford Machumu amesema upatikanaji wa maji hayo safi na salama ni historia ya kijiji hicho kwa kuwa hayakuwepo tangu enzi za uhuru wa Tanganyika na kwamba imekuwa ni faraja kubwa kwa wakazi wa kijiji hicho maji hayo yatasaidia kupunguza magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama.
Nyangi Marwa ni mzaliwa na mkazi wa kijiji hicho anasema awali walikuwa wakitembea umbali wa kilometa tano kwenda kununua maji ya mabwawa yanayouzwa shilingi 500 ndoo moja ya lita 20 tofauti na bei wanayouziwa ndoo hiyo kwa shilingi 30, aliishukuru serikali kwa kuwaboreshea miundombinu hiyo ya visima vya kisasa vinavyotoa maji kupitia mabomba.
"Zamani kabla ya mradi huu tulikuwa tukiamka alfajiri saa kumi na moja na kwenda kufuata maji mbali sana tulikuwa tunavuka vijiji vinne, hali hiyo ilipelekea ndoa za baadhi ya wanawake wenzangu kuvunjika kwa kutokuaminiwa na wanaume zao, Pia maji hayo tulikuwa tukishea na mifugo yetu na wanyama wengine wakati mwingine ni machafu yanakuwa na vinyesi hadi vya binadamu" Amesema Nyangi.