Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Agosti 16, 2025, akiwa pamoja na Viongozi wenzake wa Kitaifa wa Chama hicho, wamewasili Mkoani Simiyu Tanzania Bara, na kupokelewa na Umati mkubwa wa Wanachama, Wapenzi, Wafuasi na Wananchi kutoka Maeneo mbali mbali wa Mkoa huo.
Mapokezi hayo ambayo yamefanyika katika Kata ya Mwandoya, Jimbo la Kisesa, yakiwahusisha Viongozi hao, ni mwendelezo wa yale yaliyofanyika Agosti 09 na 10 Visiwani Unguja na Pemba, yakiwajumuisha Wagombea wa Nafasi za Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Urais wa Zanzibar.
Hayo ni Mapokezi ambayo yamekuja baada ya ACT-Wazalendo, kufuatia Wajumbe wa Mkutano wake Mkuu Maalum walioketi Agosti 06, Jijini Dar es Salaam, kuwapitisha Ndugu Luhaga Mpina na Bi Fatma Abdulhabib Ferej, kwa Nafasi ya Mgombea na Mgombea-Mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; pamoja na Mheshimiwa Othman kwaajili ya Nafasi ya Urais wa Zanzibar, katika Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Mapokezi hayo yameshuhudia zaidi ya Wanachama Wapya 1400, sambamba na Madiwani Wawili (2) waliokihama Chama Cha Mapinduzi (CCM); pamoja na Mwenyekiti wa BAWACHA, aliyekuwa Mbunge Mstaafu wa CCM na CHADEMA, na ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Maswa na Meatu, Bi Rosemary Kirigini.
Aidha, katika Mapokezi hayo, Maelfu ya Wanachama na Wananchi wa Kisesa wamejitolea kumdhamini Ndugu Mpina, ili kugombea Nafasi hiyo.