Maambukizi ya Njia ya Mkojo Yanavyowatesa Wengi Nchini

GEORGE MARATO TV
0


*Sababu,tahadhari na changamoto ya usugu wa dawa*


*Na Mwandishi wa Makala za Moto*

Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) yameendelea kuwa changamoto kubwa ya kiafya kwa watu wazima, hususan wanawake, lakini pia wanaume kwa kiwango kidogo. 

Maelfu ya wagonjwa wanafika katika vituo vya afya kila mwezi wakilalamikia maumivu wakati wa kukojoa, haja ndogo ya mara kwa mara, uchafu au harufu mbaya ya mkojo, na hata homa kali.

Wengi wa waathirika hawa hupata maambukizi yanayosababishwa na bakteria anayeitwa Escherichia coli (E. coli), ambaye ameonekana kuhusika na zaidi ya asilimia 80 ya maambukizi ya njia ya mkojo duniani kote. 

Hali hii imekuwa ya kurudiarudia kwa baadhi ya wagonjwa, na hivyo kusababisha adha ya kudumu inayohitaji matibabu ya mara kwa mara, na kwa baadhi, mpaka vipimo vya maabara kama Culture and Sensitivity ili kupatikana dawa sahihi.


E. coli: Bakteria wa kawaida anayesababisha tatizo kubwa.


Kwa kawaida, E. coli ni bakteria anayeishi kwenye utumbo wa binadamu bila madhara yoyote. 

Hata hivyo, tatizo huanza pale anapohama kutoka sehemu ya haja kubwa na kuingia katika njia ya mkojo, kuanzia kwenye mrija wa urethra, kibofu cha mkojo hadi kwenye figo.

Hali hii hujitokeza zaidi kwa wanawake kwa sababu miili yao kimaumbile huwa na urethra fupi iliyo karibu na njia ya haja kubwa. Hii hurahisisha usafiri wa bakteria kutoka sehemu ya haja kubwa hadi kwenye njia ya mkojo, hasa iwapo usafi hautazingatiwa ipasavyo.

Pia, matumizi ya nguo za ndani zinazotengeneza joto na unyevu kama nailoni, kukaa na mkojo muda mrefu, au kushindwa kunywa maji ya kutosha kunachangia bakteria hawa kujijenga kwa haraka katika mfumo wa mkojo.


Usafi duni na tabia za ngono zembe nazo huchochea maambukizi hayo.


Katika mazingira ya kawaida, maambukizi haya huweza kuzuiwa kwa njia rahisi kama kuosha sehemu za siri kwa maji safi mara mbili kwa siku, na kuhakikisha usafi sahihi baada ya kujisaidia; kwa maana kujisafisha kutokea upande wa mbele kwenda nyuma (si kinyume chake).

Hata hivyo, uchunguzi umeonyesha kuwa maambukizi ya UTI huongezeka zaidi kwa watu wanaojihusisha na ngono isiyo salama.

Wanawake wanaoshiriki tendo la ndoa mara kwa mara bila kujikinga hujikuta wakipatwa na UTI kwa kurudiarudia. Hali hii hutokana na msuguano wa tendo lenyewe kuweza kusukuma bakteria waliopo sehemu ya nje ya uke kuingia kwenye urethra.

Kujamiiana na wapenzi mbalimbali, au kufanya ngono ya haja kubwa kisha kuendelea na ya kawaida bila kuosha au kubadilisha mpira wa kinga ama kondomu, kunaongeza uwezekano mkubwa wa kuingiza bakteria wa E. coli kutoka kwenye upande wa haja kubwa hadi sehemu za mbele.

Kukojoa mara moja baada ya tendo la ndoa husaidia kupunguza uwezekano wa maambukizi kwa kusafisha bakteria waliopenya urethrani. Wanawake hasa wanapaswa kufanya hivyo kila mara baada ya tendo hilo.


*Takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa*


Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Taifa la Takwimu (NBS), kati ya mwaka 2019 hadi 2023, visa vya maambukizi ya UTI viliongezeka kutoka wagonjwa 732,500 hadi 986,400. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 34 katika kipindi cha miaka mitano.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya visa hivyo huhusisha wagonjwa wa jinsia ya kike. 

Mikoa yenye viwango vya juu vya maambukizi ni pamoja na Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya.

Takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa E. coli husababisha zaidi ya asilimia 80 ya UTI zote duniani, na usugu wa vimelea hivi kwa baadhi ya dawa unaongezeka kwa kasi ya kutisha.


*Usugu wa dawa: changamoto ya matibabu*


Tatizo kubwa kwa sasa ni kwamba E. coli ameanza kuonyesha usugu dhidi ya dawa nyingi za kawaida ambazo zamani zilikuwa zikifanya kazi vizuri. Wagonjwa wengi hujitibu wenyewe kwa kutumia dawa za kujinunulia madukani wao wenyewe pasipo kwenda kwa madaktari (Over the Counter) lakini hawapati nafuu, na hatimaye hujikuta wakienda  hospitalini wakiwa katika hali mbaya zaidi.

Taarifa kutoka Maabara Kuu ya Taifa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) zimeonyesha kuwa dawa zifuatazo zimepoteza uwezo mkubwa wa kutibu UTI kutokana na usugu wa E. coli:

1. Amoxicillin – usugu wa zaidi ya 75%

2. Ampicillin, usugu wa zaidi ya 80%

3. Ciprofloxacin, usugu wa 65%

4. Trimethoprim-Sulfamethoxazole, usugu wa 70%

5. Nitrofurantoin, usugu wa karibu 35%

Kwa wagonjwa wenye historia ya UTI ya kurudiarudia, ni lazima wafanyiwe kipimo cha Culture and Sensitivity ili kubaini dawa ambayo itamfaa moja kwa moja kulingana na aina ya E. coli aliyepo mwilini mwake.


*Njia za kujikinga na UTI zinazojirudia*


Kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba, ni muhimu kuchukua hatua zifuatazo ili kuzuia maambukizi haya:

Osha sehemu za siri kwa maji safi mara mbili kwa siku.

Safisha baada ya haja kubwa kutoka mbele kwenda nyuma.

Kunywa maji mengi, angalau lita 1.5–2 kwa siku.

Kakojoe mara unapojisikia, usizuie mkojo kwa muda mrefu.

Kakojoe mara baada ya kujamiiana.

Vaa nguo za ndani  za pamba na pia epuka nguo za kubana kwa muda mrefu.

Tumia kinga ukiwa na mpenzi mpya au zaidi ya mmoja.Lakini pia kwa mujibu wa ushauri wa na maadili ya dini, tusiwe na mpenzi zaidi mmoja.Ukishaoa au kuolewa usitoke nje ya ndoa.

Epuka kutumia dawa pasipo ushauri wa daktari, lakini pia jenga tabia ya fanya kipimo kwanza.

Fanya uchunguzi wa mara kwa mara hasa kwa walioathirika mara nyingi

UTI zinazojirudia huathiri ubora wa maisha kwa kiasi kikubwa.

Zinapunguza uwezo wa mtu kufanya kazi, husababisha maumivu ya mara kwa mara, na kwa baadhi, huweza kusababisha maambukizi kwenye figo, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya muda mrefu.

Watanzania wanapaswa kuacha kutumia dawa kiholela na badala yake kufuata utaratibu wa kitaalamu wa vipimo kabla ya matibabu. Serikali nayo inapaswa kuimarisha upatikanaji wa vipimo vya Culture and Sensitivity katika hospitali za mikoa na wilaya ili huduma hii isibaki kwa wenye uwezo tu.

Wakati dunia inakabiliana na tishio la usugu wa dawa, hatua binafsi na elimu kwa jamii ndiyo silaha madhubuti ya kupunguza ongezeko la maambukizi haya.


*_Mwandishi wa  Makala za Moto ameandika makala haya baada kufanya utafiti wa mwezi nzima katika akihojiana na Madaktari Bingwa mbalimbali wa Idara ya Magonjwa ya Njia ya Mkojo (Urolojia) wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.Pia amesoma machapisho mbalimbali ya Afya na Tiba_*

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top