Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini anayemaliza muda wake na mtia nia wa Ubunge wa Jimbo jipya la Uyole kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, leo tarehe 2 Agosti 2025, amejitambulisha rasmi kwa Wajumbe wa Mikutano ya Kata mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi wa ndani wa CCM unaotarajiwa kufanyika Jumatatu, tarehe 4 Agosti 2025, nchi nzima.
Katika mikutano hiyo, Mhe. Dkt. Tulia amewaomba Wajumbe hao kumpigia kura nyingi za ndiyo ili kupata ridhaa ya kuwawakilisha na kuwatumikia wananchi kupitia nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Uyole. Amewaeleza dhamira yake ya kuendeleza jitihada za maendeleo na kuhakikisha jimbo hilo linapata uwakilishi wenye tija na ufanisi.
Kata alizotembelea ni pamoja na Mwakibete, Ilomba, Ilemi, Isyesye, na Itezi, ambapo aliwasilisha vipaumbele vyake vya maendeleo ikiwemo kuboresha huduma za elimu, afya, miundombinu na ustawi wa jamii kwa ujumla.