Wafukua kaburi na kusepa na kichwa

GEORGE MARATO TV
0


Na MASHAKA MHANDO, Tanga

JESHI la polisi mkoani Tanga, linafanya uchunguzi wa kuwasaka watu waliohusika  kufukua kaburi na kukata kichwa cha marehemu aliyezikwa na kundoka nacho.

Akizungumza ofisini kwake Leo Julai 20, Kamanda wa polisi mkoani Tanga, ACP Alimachius Mchunguzi alisema jeshi hilo linafanyia uchunguzi taarifa za watu kufukua kaburi na kundoka na kichwa na kubakisha mwili kwenye kaburi.

Akifafanua Kamanda Mchunguzi alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 18 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi baada ya wananchi kutoa taarifa za kufukuliwa kaburi la mtu mmoja aliyezikwa katika makaburi ya familia Julai 12 mwaka huu katika Kijiji cha Mgela kilichopo wilayani Kilindi.

Kamanda Mchunguzi alimtaja marehemu huyo kwa jina la Mohamed Athumani Mjaila (85) ambaye alifariki dunia Julai 11  na kuzikwa siku iliyofuata katika makaburi yao ya ukoo  katika Kijiji hicho.

"Ni kweli tukio hilo limetokea Julai 18 majira ya asubuhi huko katika Kijiji cha Mgela kwenye makaburi ya familia ambako walikuta watu wamefukua na kundoka na kichwa," alisema.

Kamanda alisema awali Wananchi waliona kaburi limefukuliwa wakahisi kwamba huenda watu hao wameondoka na mwili wote lakini walipofukua kujiridhisha, walikuta inekatwa kichwa ambacho waliondoka nacho na kubakisha mwili kwenye kaburi hilo.

Alisema familia na jeshi hilo wanahisi ni Imani za kishirikina lakini Polisi wameanzisha uchunguzi wa kuwasaka wahusika ili wawafikishe katika vyombo vya sheria.

Kamanda huyo wa polisi hata hivyo alisema jamii iepuke kushiriki kwenda kwa waganga ambao wanafanya au kupiga lamli chonganishi ambazo hazina msingi wowote badala yake wanavunja sheria kwa kufanya mambo yanayoleta taaruki kwa jamii.

"Tunafanya uchunguzi kujua ni akina nani wamefanya tukio hilo ambalo watu wanahisi ni mambo ya ushirikina ambayo hayasaidii kwenda kwa waganga wanaofanya lamli chonganishi ni utapeli na ni matendo yasiyokuwa ya ubinadamu," alisema Kamanda Mchunguzi.

Kamanda wa polisi alitoa wito kwa Wananchi kushirikiana na jeshi hilo ili kuwabaini wahusika wa tukio hilo ili wafikishwe kwenye vya sheria kukomesha matukio hayo.

Tukio hilo limeacha simanzi kubwa kwa Wananchi wa Kijiji hicho hasa watu wa Familia hiyo wakieleza kwamba waliofanya tukio hilo wamewakumbusha na kuwapa majonzi zaidi kwa kuondokewa na ndugu yao.

"Tunaimani na jeshi la polisi watachukuza watawakamata na watatupa majibu watu waliofanya kiukweli wametupa majonzi kwasababu arobaini ya mpendwa wetu bado haijafanyika tayari wameondoka na kichwa na ndugu yetu," alisema Msekwa Mjaila mmoja ya wanafamilia wa marehemu huyo. 




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top