Na MASHAKA MHANDO, Horohoro
SERIKALI za Tanzania na Kenya zinakwenda kuimarisha diplomasia ya kidijitali, biashara na uchumi baada ya kuzindua mkongo wa mawasiliano baina ya nchi hizo.
Wakizindua mkongo huo Leo Julai 18 Waziri wa Mawasiliano na teknolojia ya Habari Jerry Silaa alisema uzinduzi wa maunganisho ya mkongo wa Taifa wa mawasiliano (NICTBB) wa TTCL na mikongo ya bahari iliyopo Mombasa kupitia ICTA Kenya katika eneo la Horohoro wilayani Mkinga mkoani Tanga, utakuwa na faida kubwa kwa wananchi.
Alisema kupitia mkongo huo wananchi wataweza kupata huduma nafuu ya mtandao ambayo itasaidia kuimarisha shughuli za kibiashara na uchumi kutokana na kuimarika kwa miundombinu hiyo ya mawasiliano itakayokuwa na kasi zaidi.
"Tunakwenda kuangalia sera zetu katika maeneo ya kutolea huduma baina ya nchi zetu ili wananchi waweze kupata huduma bora za mawasiliano lakini zinazozingatia maadili na weledi"alisema Waziri Silaa.
Alisema kazi ya kujenga miundombinu ya nchi zinazoshirikiana ni ya nchi zote kwa pamoja, lakini pia kuna faida kubwa ya kuunganisha na mikongo mingi kwani husaidia kuwepo kwa mtandao wa uhakika.
Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na uchumi wa kidijitali Kenya William Kabogo Gitau alisema mkongo huo utaweza kuimarisha ubunifu wa kiteknolojia kwa wananchi wa nchi hizo
“Vijana wetu ambao wamebobea katika mambo ya uhandisi na ubunifu watakwenda kuongeza ujuzi wao kutokana na kuimarika kwa huduma hiyo ya mtandao na hivyo kufungua fursa mpya ya maendeleo kupitia teknolojia ya kidijitali”alisema Waziri Gitau
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara yaawaaioiano, Teklonojia ya Habari, Mhandisi Leo Magomba alisema kuwa tayari wilaya 109 kati ya 131 zilizopo nchini zimeweza kuunganishwa na huduma ya mkongo wa taifa ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wilaya zilizobaki zitaunganishwa na huduma hiyo.
“kupitia Mkongo huu tunakwenda kuboresha huduma ya mawasiliano kikanda lakini sasa nchi yetu inakwenda kuwa kitovu cha mawasiliano yenye ubora ndani na nje ya nchi”alisema Mhandisi Magomba
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Mawasiliano la Tanzania TTCL Moremi Marwa alisema kuwa mkongo huo utaweza kuimarisha mawasiliano baina ya nchi hizo mbili sambamba na kikanda.
Alisema kuwa awamu ya kwanza ya mkonga huo imeweza kuunganisha nchi sita za Afrika ya Mashariki huku hatua ya pili ni kuunganisha huduma hiyo katika nchi ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo DRC.
Alizitaja nchi hizo kuwa ni Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, Msumbiji na Uganda ambao wameunganishwa na mkongo huo wa Tanzania na changamoto ya kukatika mawasiliano itakuwa imefikia kikomo.
“Mpaka sasa nchi yetu imeweza kuunganishwa na huduma ya mikongo nane ya mawasiliano ambayo inatoa uhakika wa huduma bora ya mtandao pindi inapotokea njia moja wapo imepata hitilafu, wananchi hawawezi kuona tatizo hilo kwakuwa huduma itaendelea kupatikana," alisema Marwa.
"Mambo ya kuzingatia, ni mashirikiano kwa nchi zote mbili, kutunza miundombinu hiyo ili kuepuka uharibifu na kuleta changamoto ya kukatika kwa umeme na mtandao, lakini pia tuendelee kuwa na mahusiano ya karibu" amesema Waziri Gitau.
Katika hatua nyingine mbunge wa Lungalunga nchini Kenya Mangale Chipolomondo na mwenyekiti wa bodi ICT nchini humo Lily Ng'ok wamesikitishwa na matumizi mabaya ya mtandao uliotumiwa na vijana wa Kenya kuwatusi viongozi wa Tanzania.
Wakizungumza kwenye uzinduzi huo, Wakenya hao walitumia fursa hiyo kuwaomba radhi Watanzania na serikali kwa vijana wa Kenya kutumia mitandao kuwatusi viongozi wa Tanzania akiwemo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
"Tusitumie mitandao vibaya kuwatukana viongozi, wale waliofanya vile ni mitizamo yao lakini sisi na Tanzania ni ndugu na uzinduzi huu unazidi kutuweka pamoja kijiditari," alisema Mangale.
Mwenyekiti wa bodi ya ICT nchini Kenya alisema vijana waitumie mitandao kwa matumizi yenye faida wasitukane viongozi kama ambavyo vijana wa Kenya walivyofanya.
"Sisi hatuko nao pamoja ni wao wenyewe wametumia vibaya mitandano kuwatusi viongozi na tunaomba radhi kwa hili na tuendelee kudumisha Umoja tuliokuwa nao," alisema mwenyekiti huyo.