Lema Atoa Maneno Mazito Dhidi ya Mbowe

GEORGE MARATO TV
0


 Anaandika Godbless Lema kwenda kwa Mbowe.


Kwako Mh Freeman Mbowe.

Kwa heshima, huzuni na uzito wa dhamira, nakuandikia barua hii si kwa hasira, bali kwa mwangwi wa historia inayolilia uaminifu. Tulisimama nyuma yako kwa gharama kubwa kipindi chote ambacho tulikuamini kuwa kiongozi wa matumaini ya kizazi kilichojitoa kwa ajili ya Tanzania mpya ulipokuwa Mkti wetu.

Leo hii umetazamwa ukihudhuria mkutano wa Serikali kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa, huku mwenyekiti wetu, Tundu Lissu, akiwa gerezani akikabiliwa na mashtaka ya uhaini na Chama chetu hakiruhusiwi kufanya siasa na wanachama wetu wanapotea, wanateswa, wengine wameuawa na bado hujatokea hata mara moja mahakamani, wala kutoa neno la kukemea udhalimu huu unaoendelea mbele ya macho ya Watanzania.

Tulikuwa pamoja nawe wakati ulipokamatwa na kushtakiwa kwa ugaidi na changamoto mbali mbali nyingi katika uongozi wako. Tulilia. Tulipiga kelele. Tulivunjwa. Tukateswa. Lakini tuliendelea kusimama kwa ajili yako kwa sababu tuliamini ulikuwa kiongozi wa haki. Leo, unajibu kwa ukimya. Ukimya usio na ujasiri. Ukimya unaogharimu damu nyingine isiyo na hatia.

“Mungu hadhihakiwi; kwa maana apandacho mtu ndicho atakachovuna.”

Wagalatia 6:7

Kaka, imekuwa ikisemwa kwamba unayo hasira dhidi ya baadhi ya maneno yaliyotamkwa na wanachama wakati wa uchaguzi wa ndani wa chama. Lakini je, unaweza kweli kuwa na hasira dhidi ya maneno hayo ya kawaida kuliko kuwa na hasira dhidi ya waliokufunga kwa kukuita gaidi? Je, unaweza kuwa na uchungu kwa wakosoaji wako wa ndani, lakini ukaishi kwa amani na wale ambao walikutesa na tunao washutumu kwa utekaji, mateso, vifo na dhuluma dhidi ya haki na utu?

Ulikuwa Mwenyekiti kwa zaidi ya miaka 20. Siwezi kuandika hapa majina ya watu waliopoteza maisha kwa sababu waliamini kuwa uongozi wetu ulikuwa na dhamira ya kweli. Tumewazika karibu kila mkoa wa nchi hii, tumewasaidia majeruhi. Tumewaokoa wachache gerezani. Na wengi wao walipigania jina lako. Waliamini katika mfumo uliouongoza. Leo hii, je tuseme nini kwa familia zao? Wakati wao bado wanalipa gharama ya mapambano . 

Wakati huo huo, hujawahi hata siku moja kusema au kuandika hadharani kuhusu mateso haya yanayoendelea kwa CHADEMA na viongozi wake haswa kesi mbaya inayo mkabili Mkti wetu Tundu Lissu.

“Kama sauti ya damu ya Abeli ililia kutoka ardhini, ndivyo sauti ya mashujaa wa haki inavyolia kila siku ikitafuta si kisasi, bali uaminifu wa dhamira.” Mwanzo 4:10

Kama tuliweza kuamka kwa ajili yako, ulipokuwa kiongozi wa Chama chetu , kwanini sasa usiweze kusimama kwa ajili ya haki , maana hata Kama unapumzika siasa lakini binadamu mwema hawezi kupumzisha dhamira yake juu ya haki na utu. Unafikiri ni sahihi kukosekana kwa andiko au sauti na uwepo wako Mahakamani toka Lissu amekamatwa na kwa ajili ya wengine wengi ambao sasa wako katika hatari kubwa ?  

Chama ambacho wewe ni Mjumbe wa Kamati Kuu hakiruhusiwi kufanya mikutano ya hadhara. Vijana wake wanapigwa. Mwenyekiti wake yuko jela na viongozi wake wanateswa. Na bado, hakuna neno kutoka kwako. Hakuna kilio na bado unaweza kushiriki hafla za Serikali bila aibu. Nini kiko nyuma ?

“Dhamira safi huwa haipumziki katika meza ya heshima, ikiwa vunjiko la haki linapiga kelele mlangoni.” 


Nelson Mandela

Kwa heshima na unyenyekevu wa historia, tunakuomba , usijitenganishe na damu ya mashujaa waliokuamini.

Usikubali jina lako kuwa ukuta wa kusahau damu ya wale waliochinjwa kwa jina la mabadiliko.Usikubali kusimama upande wa utulivu bandia unaozima sauti ya walalia haki.

Huu si mwaliko wa ugomvi. Hii ni sauti ya dhamira. Kilio cha kizazi kilichoumizwa, lakini bado kinabeba matumaini kwamba kuna waliotumwa kusimama kwenye ufa wa taifa.

“Haki haipotei, hata ikizikwa kwenye vumbi la kisiasa huibuka tena kwa sauti ya waliojeruhiwa.”

Na hata kama haukumbuki vilio vya waliopotea, kumbuka hili ,mahali ambapo Tundu Lissu anateseka leo Mahakama Kuu ya Tanzania si mbali sana kama Dodoma ulipokuwa ukishiriki kwenye mkutano wa Serikali.

Ni safari ya dhamira tu inayotenganisha hatua zako na hatua ya haki.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top