Kampeni ya "Badilika, Tokomeza Ukatili"

GEORGE MARATO TV
0

 



Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amezindua rasmi kampeni ya 'Badilika, Tokomeza Ukatili' itakayotekelezwa kwa miaka miwili 2025/27 mkoani Kigoma.

Akizindua kampeni hiyo iliyoandaliwa na shirika la maendeleo la nchini Ubelgini ENABEL katika uwanja wa Mwanga Centre mkoani Kigoma Jumatatu Julai 28, 2025, Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito kwa jamii kubadili tabia, mitazamo na mienendo inayochochea ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Amesisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kuwa sehemu ya mabadiliko huku akijiunga mwenyewe kama balozi wa mabadiliko na Kampeni ikilenga kuvuna mabalozi 150,000 katika mkoa huo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msukumo mkubwa katika kutokomeza ukatili kupitia sera madhubuti na mikakati ya kitaifa kama Sera ya Taifa ya Jinsia ya mwaka 2023 na Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II).

Aidha Waziri Dkt. Gwajima amelipongeza Shirika la ENABEL kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine ikiwemo shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI katika mapambano dhidi ya ukatili.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zimesaidia kuwawezesha wanawake na wasichana kupitia miradi ya maendeleo kama vile mradi wa “Wezesha Binti” unaotekelezwa mkoani Kigoma na hivyo kuwa mfano bora wa namna vijana wa kike wanavyopatiwa elimu, ujuzi na fursa za ajira.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubelgiji ENABEL, Koen Goekint ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa na namna ilivyopokea kampeni hiyo huku akihaidi ushirikiano zaidi katika juhudi za kutokomeza ukatili wa kijinsia, kulinda usawa wa kijamii na kuwezesha wanawake kiuchumi na kijamii.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Michael Ngayanila amesema kupitia kampeni hiyo watahakikisha wanaifikia jamii ili kuhakikisha kila mmoja anakuwa anachukua hatua za kuzuia ukatili kabla haujatokea.

Akiongoza mdahalo wakati wa ufunguzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI, Yassin Ally amesema jitihada zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia na wadau wa maendeleo zimesaidia ukatili wa kijinsia kupungua mkoani Kigoma kutoka asilimia 61 mwaka 2016 hadi asilimia 34 mwaka 2025 huku mimba za utotoni zikipungua kutoka asilimia 32 hadi asilia 17.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akiwa na viongozi mbalimbali wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili mkoani Kigoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza wakati wa uzinduzi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Michael Ngayanila akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Kigoma, Simon Siro.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ubelgiji ENABEL, Koen Goekint akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili inayotekelezwa mkoani Kigoma.
Meneja Mradi wa Wezesha Binti unaotekelezwa na shirika la ENABEL, Christine Rankote akitoa maelezo kuhusu mradi huo ambapo amesema lengo ni kuwafikia wanamabadiliko 150,000 hadi kufikia mwaka 2025 ambapo kila mmoja anatarajia kuwafikia wananchi watatu na hivyo jumla ya wanufaika wa mradi kuwa 450,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI, Yassin Ally (kulia) akiongoza mdahalo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili mkoani Kigoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima (mwenye kofia) akiwasili uwanja wa Mwanga Centre mkoani Kigoma kuzindua kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za watoto na wanawake KIVULINI, Yassin Ally (mwenye kofia) akiwa na wananchi wakifurahia uzinduzi wa kampeni ya Badilika, Tokomeza Ukatili.
Wadau mbalimbali wakiwa na mabango yenye kuhamasisha jamii kutokomeza ukatili.
Wadau wakiwa kwenye uzinduzi huo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top