Ccm inatoa Somo Duniani Uimara Wake, Kujibadilisha Kuendana na Wakati

GEORGE MARATO TV
0


_Kudijitilize Chama, kurekebisha Katiba kuendana na mahitaji ya sasa._


Na Bwanku M Bwanku.

Moja ya sifa kubwa inayoweza kuifanya taasisi yoyote duniani kuendelea kuishi, kuwa imara na kushawishi kundi kubwa la watu basi ni uwezo wake wa kubadilikabadilika kulingana na muda na mahitaji ya wakati uliopo wa watu inaowahudumia. Lazima ubadilike kwenda na muda (dynamic) na sio kung'ang'ania ujima (static).

Mtaalamu wa masuala ya taasisi (Organizational Structure) Mjerumani Max Weber aliwahi kusema kwamba taasisi isiyobadilika na inayokumbatia uhafidhina (conservative) inajiandalia kifo chake yenyewe.

CCM ni moja ya Chama kikongwe na kikubwa sana sio tu Afrika bali duniani kikishiba utajiri mkubwa wa kihistoria na kitaasisi. Ni Chama cha Pili kwa ukubwa, cha muda mrefu na kikongwe zaidi Barani Afrika baada ya Chama Cha True Whig Cha Liberia kikiwa na miaka 48 toka kiasisiwe Februari 05, 1977 baada ya kuunganika kwa Vyama viwili vya Tanganyika African National Union (TANU) cha Tanganyika kilichokuwa chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Afro-Shirazi Party (ASP) cha Zanzibar kilichokuwa chini ya Sheikh Amaan Abeid Karume.

Inasifika na kufahamika kama Chama Kikuu Cha Ukombozi Kusini mwa Afrika hasa kwa mchango wake mkubwa wa kusaidia Mataifa mengi sana Kusini mwa Afrika kupata Uhuru wake na kujikomboa kutoka kwa Wakoloni. Miaka ya 1977's, CCM ikiwa chini ya Hayati Mwalimu Nyerere kama Mwenyekiti wake kilisaidia sana kwa hali na mali Mataifa mengi ya Afrika kama Zimbabwe, Msumbiji, Zambia, Angola, Afrika Kusini na mengine mengi kupigania na hatimaye kupata Uhuru wake kutoka kwa Wakoloni.

Kwa ukubwa wa kitaasisi na kihistoria na umri wa miaka 48 ulionao, suala la CCM kubadilikabadilika kuendana na wakati, mahitaji ya muda husika na kuangalia watu inaowahudumia ni jambo lisilopingika ili kuifanya taasisi iendelee kuaminika zaidi kwa watu. 

CCM imeendelea kubadilikabadilika kuendana na mahitaji ya muda husika, ilipoonekana wajumbe wanaopiga kura za maoni ni wachache sana hivyo kuchochea rushwa CCM ilifanya Marekebisho ya Katiba yake kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Taifa wa Januari 18 na 19, 2025 na kuongeza idadi ya wapiga kura za maoni ili kutoa wigo mpana kwa wanaCCM kuchagua mtu anayekubalika. 

Pia, ilipoonekana majina matatu ni machache kupigiwa kura za maoni hasa kwa kuangalia jinsi wanaCCM wengi wenye sifa tofauti tofauti walivyojitokeza kuchukua fomu, CCM imebadilika haraka na kufanya Marekebisho ya Katiba yake na kuongeza idadi ya majina kuwa zaidi ya matatu.

Na wiki hii, jana Jumamosi Julai 26, 2025 CCM imeandika historia ya kuwa Chama cha kwanza Afrika kufanya Mkutano Mkuu wake Maalum uliofanya maamuzi mazito yanayokiletea mageuzi makubwa Chama kupitia njia ya mtandao kikikutanisha Wajumbe wake 1915 kati ya 1931 wa Mkutano Mkuu kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania. 

Hili si tu limefanya mageuzi makubwa ya kidijitali kukutanisha wanaCCM nchi nzima kwa njia ya mtandao lakini Mkutano Mkuu huu Maalum umefanya mabadiliko madogo ya Katiba ya CCM ili kuendana na nyakati hizi tulizonazo. Nimeandika hapa, uhai na uimara wa taasisi yoyote ile duniani basi ni uwezo wake wa kubadilika haraka kulingana na wakati, watu inaowahudumia na mahitaji ya muda husika na sio kukumbatia uzamani. 

Kwa Mujibu wa Mwenyekiti wa Chama hiki na Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Mei 28 na 29 mwaka huu alisema hadi kufikia Mei 29 mwaka huu, idadi ya wanachama wa chama hicho ni Milioni 13, 000, 670. Wanachama hawa wote wako kwenye kanzidata ya pamoja kwenye mfumo wake wa CCM APP na wote wanatambulika popote walipo na wanapewa kadi ya kisasa ya kielektroniki.

CCM ni moja ya Chama kinachoongoza kwa kua na wanachama wengi Barani Afrika na ina utajiri mkubwa sana wa wanachama humo ndani kuna wasomi wakubwa, maprofesa, madaktari na kila aina ya wanachama wenye sifa tofauti na wanaotaka kutumikia wananchi kwa njia mbalimbali au kushiriki maamuzi muhimu ndani ya Chama. 

Ili kuendana na mahitaji ya sasa na kuhakikisha kila mwanaCCM anakua sehemu ya maamuzi muhimu ndani ya Chama, ikafanyia marekebisho kidogo kwenye Katiba yake ili kuongeza wigo wa idadi ya wanachama wanaopiga kura kuamua wagombea ubunge na udiwani.

Katika dhana ileile ya kubadilika haraka kwenda na muda na mahitaji ya watu unaowahudumia, kwenye Mkutano Mkuu wa CCM wa Januari 18 na 19, 2025 uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma palifanyika Marekebisho ya Katiba ya CCM kwenye Ibara ya 47 (1), 60 (1) na 73 (1) ambapo Wajumbe wanaopiga kura za maoni waliongezwa kutoka wale wa mwanzo. Lakini pia marekebisho mengine yalikua yale ya kurudisha majina matatu tu kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni.

Mfano, lipo Jimbo lilikua na wapiga kura za maoni labda 800 lakini kwa mabadiliko haya Wajumbe walifika zaidi ya Elfu 10. Vivyo hivyo kwa upande wa udiwani wapiga kura za maoni waliongezwa na kuwa wengi zaidi. Hii inapunguza rushwa kwani Wajumbe wachache ilikua rahisi kwa wachache wasio waadilifu watafuta uongozi kwa fedha na rushwa kuwafikia lakini leo jimbo lina mpaka wapiga Elfu 10 hapo hata mtoa rushwa lazima achemke.

Wajumbe sasa wa kupiga kura za maoni wengi zaidi na mabadiliko hayo yanakwenda katika utaratibu wa kuchuja wagombea na itapandisha ngazi ya juu wagombea watatu labda kamati itaona vinginevyo. Lengo likiwa kuongeza ushiriki wa wanachama kufanya maamuzi, kutanua wigo wa demokrasia kwa wanaCCM, kuimarisha muundo wa ngazi ya shina pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Baada ya kupitisha mabadiliko yale ya kuruhusu majina matatu tu kwenda kupigiwa kura za maoni, pamekua na maoni mengi ya wanachama na wananchi kuhusu uchache wa majina ya kupigiwa kura za maoni hasa ukizingatia CCM ina utajiri mkubwa sana wa wanachama na tumeona jinsi makundi mengi ya wasomi, watumishi, wanamuziki, wachekeshaji, waigizaji yalivyojitokeza kuchukua fomu kuomba nafasi za ubunge na udiwani mwaka huu 2025.

Katika kubadilikabadilika kwenda na wakati, tena CCM imerudi kwenye Mkutano Mkuu wa CCM kufanya marekebisho madogo ya Katiba yake ili kwenda na nyakati na aina ya watu inaowahudumia. 

Na marekebisho ya Katiba kwenye upande wa majina ya watu walioomba kugombea ubunge na udiwani ambapo licha ya majina ya wagombea wanaoteuliwa ngazi ya Kamati za Siasa za Wilaya na Mkoa kubaki matatu kwa kila Jimbo na Kata, kwa marekebisho haya madogo ya Katiba, Kamati Kuu itakuwa na uwezo wa kubadilisha maamuzi endapo itaamua vinginevyo.

Akisoma marekebisho hayo kwenye Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika kwa njia ya mtandao Jana Julai 26, 2025 Jijini Dodoma, Katibu wa NEC- Organizesheni Issa Haji (Gavu), amesema Marekebisho yaliyofanyika na kubarikiwa na Mkutano Mkuu huu ambao ndicho chombo chenye mamlaka kufanya hivyo ni Marekebisho ya Katiba ya CCM Ibara ya 105 ibara kuu ya 7 F kwa kuongeza maneno  "isipokuwa kama Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itaamua vinginevyo."

Hivyo Ibara ya 105 ibara kuu ya 7 F ya CCM inapendekezwa isomeke kama ifuatavyo "Kufikiria na kuteua majina ya Wana CCM wasiozidi watatu kwa kila Jimbo la uchaguzi walioomba nafasi ya Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi ili wakapigiwe kura isipokuwa kama Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itaamua vinginevyo."

"Kwa upande wa udiwani inapendekezwa kufanya marekebisho kwenye ibara ya 91 6C  kwa kuongeza maneno isipokuwa kama Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itaamua vinginevyo hivyo mapendekezo yatasomeka "kwa upande wa udiwani itafikiria na kuteua majina ya Wana CCM wasiozidi watatu kwa kila Kata ili wakapigiwe kura za maoni isipokuwa kama Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itaamua vinginevyo."

Marekebisho haya yote yamepitishwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika kwa njia ya mtandao kwa asilimia 99.8 na sasa yanatumika rasmi. 

Marekebisho haya yote ya Katiba ya CCM yanakifanya Chama kuendana na hali ya sasa ya Chama ili kutoa fursa kwa wanaCCM wengi zaidi. Na hii inadhihirisha CCM inavyotoa darasa la kubadilikabadilika haraka kuendana na mahitaji ya wakati husika na watu inaowahudumia.

Ukubwa wa historia yake, kitaasisi kubadilikabadilika kulingana na wakati na mahitaji ni jambo lisilopingika kwa CCM ili kuendelea kuimarika na kuaminiwa zaidi na kwenye hili imethibitisha kwa vitendo.











*MAKALA HII IMEANDIKWA NA NDUGU BWANKU M BWANKU. KWA MAONI, USHAURI ANAPATIKANA KWA EMAIL bwanku55@gmail.com

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top