Ada Ouko, Musoma.
MKAZI wa kata ya Kwanga 'A' Wilson Omollo anashikiliwa na Jeshi la polisi mkoani Mara kwa tuhuma za kuanzisha kituo cha kutolea huduma za afya bila kuwa na kibali.
Akizungumza na GMTV leo juni 9, mwaka huu 2025 Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo(DMO) Mustapha Waziri amesema katika utaratibu wa kawaida unaotekelezwa na Manispaa hiyo wiki iliyopita walifanya ukaguzi ili kubaini vituo visivyo rasmi vinavyotoa huduma ya afya kwa jamii.
"Kwenye utaratibu wetu wa kawaida tukagundua kuna sehemu nyingi ambazo zinatolewa huduma ya afya bila kufuata utaratibu hiyo ni sehemu ya pili, sehemu ya kwanza mtaa wa Kigera, kuna mama mmoja mkunga wa jadi tulikuta ana wajawazito watatu anawazalisha nyumbani kwake"Anasema na kuongeza
'' Kwa tukio hili la leo tulipokea taarifa kwamba kuna Zahanati bubu maeneo haya na ni kweli huyu mzee ni daktari mstaafu tumekuja hapa tumekuta ana wagonjwa watano, mmoja amelazwa akiwa amewekewa dripu dirishani, alafu tumekuta watoto wawili walipata ajari ya pikipiki mmoja anaonekana amevunjika mguu wakiwa wanapatata huduma, pia tumewakuta wamama wawili ambao nao wamekuja kuhudumiwa na wametueleza walikuja kupima malaria, pia (slide) vipimo vya malaria alikuwa navyo lakini darubini hatukuiona alisema Waziri.
Amesema kuwa ili mwananchi aweze kuanzisha kituo cha kutolea huduma za afya ni lazima afuate utaratibu na kizingatia sheria zinazotakiwa jambo ambalo mzee Omollo hakulizingatia wala kulifuata.
" Hapa analaza wagonjwa, anawachoma sindano pia hana kifaa cha kuchomea taka( incenilator) sindano alizotumia kwa wagonjwa wake amezijaza humu ndani anatoa huduma kiholela hata sehemu ya kunawa mikono hana kwa mantiki hiyo ni rahisi sana kuambukiza watu ukimwi na magonjwa mengine ya kuambukizwa alisema.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kuwa mhe,Rais Samia Hassan amewekeza sana kwenye sekta ya afya kwa kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya kwa jamii kama vile Hospitali, Kituo cha afya, na zahanati huku akiwataka wana nchi kufika maeneo hayo kwa lengo la kupata huduma hiyo na maeneo mengine yaliyohalarishwa kutoa huduma hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji wa kata hiyo, Mtendaji wa kata ya Kigera Jenny Lameck anasema mzee Omollo awali alikuwa ana duka la madawa ambalo alifungiwa baada ya kugundulika kuwa analaza wagonjwa kwenye duka hilo.
" Tumeshirikiana na DMO, viongozi wengine na polisi katika upekuzi tumekuta vifaa tiba anavyovitumia kutolea huduma ya afya vikiwa kwenye mazingira yasiyo rafiki ndani ya chumba kimoja anachotumia tumekuta wagonjwa watano huku mmoja akiwa amelazwa kitandani ametundukiwa dripu la maji, wengine wawili ni watoto waliopata ajari ya pikipiki, na wanawake wawili waliokuja kupima malaria" amsema Jenny.
Kwa upande wake Mtuhumiwa huyo Wilson Omollo anaeleza, kuwa alianza kutoa huduma hiyo kwa kipindi cha miezi mitano iliyopita baada ya kufungiwa duka madawa na kwamba anatumia leseni ya duka hilo ambayo pia imekwisha muda wake.