Museveni na Mkewe waomba radhi kwa makosa waliyotenda miaka 39 ya uongozi wao

GEORGE MARATO TV
0

RAIS wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni pamoja na mkewe Janet Museveni,wameomba msamaha kwa wananchi wa Uganda kwa makosa ambayo wametekeleza katika kipindi cha miaka 39 ya uongozi wao.

Kwenye Video ambayo ilipakiwa na NTV Uganda, wawili hao walionekana kuwa wanyenyekevu na kuonyesha huruma kwa kuomba msamaha huo, wakiwa kwenye jukwaa.

 “Kama viongozi wa juu katika taifa hili, kwa unyenyekevu tunachukua jukumu la kuwajibikia makosa yote yaliofanywa na sisi wenyewe, mawakala wetu na wawakilishi wetu… Tunasimama hapa kutubu na kuwaomba msamaha, hasa watu wa Buganda na wananchi wote,” walisoma kwa pamoja ujumbe wao.

Hata hivyo, wachanganuzi hawakukosa kuchambua kwamba huku Museveni akiomba radhi kwa makosa yakijumuisha ukatili kwa wananchi, mwananchi mmoja hasa, mwanasiasa wa Upinzani Kizza Besigye angali anahangaika jela baada ya kukamatwa kikatili akiwa Nairobi na kusafirishwa Uganda.

Katika kipindi fulani majuma kadhaa yaliyopita, picha cha kudhoofika kiafya kwa mpinzani huyo ambaye zamani alikuwa daktari wake binafsi zilisambaa ikibainika kwamba alikuwa kwenye mgomo wa kula akilalamikia kuwekelewa makosa kwenye kesi hiyo.

Kwenye ombi lao, Museveni na mkewe Janet walitaka Mwenyezi Mungu kuwaonea huruma ambayo walitaka kuirejesha kama hapo mwanzo. Viongozi hao wawili walitaka waliokosewa nyoyo zao zipate uponyaji ili kuwawezesha kujumuika nao tena.

“Nyoyo za waliokosewa ziweze kupata uponyaji ili tuweze kujumuika pamoja na kuleta amani itakayotusaidia kuimarisha maendeleo jamii na uchumi,” walisema kwa pamoja Bw na Bi Museveni.

Ombi la wawili hao limeweza kukubaliwa na ufalme wa Buganda ambao wamemtaka kiongozi huyo kurejelea programu kumi za maendeleo aliyokuwa ameazisha.

Kulingana na Msemaji wa ufalme wa Buganda Bw Israel Kizibwe Kitooke, amemtaka rais huyo kukumbuka programu hizo, iwapo anataka uungwaji mkono kutoka kwa jamii ya Baganda.

 “Tumeona watu mbalimbali na tofauti wakinyakua ardhi, kuwafukuza wamiliki na hata utekaji nyara ambao unaendelea katika nchi hii ambao unahatarisha maisha ya watu wa Uganda,Mfalme wa Buganda hukubali ombi la kila mmoja ambaye huomba msamaha na ambalo huwa miongoni mwa kanuni zetu za kiutamaduni,” alisema Bw Kitooke.

Kwenye mitandao ya kijamii, kuna wale wamemtaka Rais huyo kujiuzulu iwapo msamaha wake ulikuwa wa kikweli.

“Museveni hawezi kuomba msamaha wa kikweli kwa Uganda, labda kuna kitu kipya ambacho anapanga. Waganda wanafaa kuwa makini na mbinu hiyo mpya,” alisema Caleb Musiimenta.

“Huu msamaha unahusishwa na uchaguzi ujao wa mwaka 2026. Hii ni njia moja ya kutafuta uungwaji mkono katika uchaguzi huo,” alisema Sarah Ayii.

Ombi la Rais Museveni limekuja baada ya kupoteza uungwaji mkono kwa Jamii ya Buganda kutokana na kukiuka makubaliano kadhaa ikiwemo kurejesha Mali za ufalme wa Jamii hiyo zilizokuwa zimetwaliwa na serikali zilizopita. 

Katika uchaguzi Mkuu uliopita,Museveni alipata kura millioni 1.2 kutoka Jamii ya Buganda huku mpinzani wake Robert Kyagulanyi maarufu Boby wine akipata kura millioni 2.8 kutoka kwa Jamii hiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu nchini Uganda.

Aidha Chama cha NRM cha kwake Museveni kiliambulia viti vitano vya ubunge katika Jamii ya Buganda huku Chama cha NUP cha kwake Boby wine kikipata viti 50 vya ubunge ambapo katika uchaguzi huo, Mawaziri wote zaidi ya kumi wa Museveni kutoka eneo la Buganda walipoteza viti vyao vya ubunge. 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top