Kaimu Mratibu wa Polisi Jamii Wilaya ya Magu, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Magazine Msaidizi wa Polisi Makoye Kitula, ametoa wito kwa wanafunzi wa Chuo cha Mipango kituo cha Mafunzo Mwanza kilichopo Kata ya Kisesa, wilayani Magu kuzingatia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na simu za mkononi kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.
Mkaguzi Kitula ametoa wito huo Jana Jumatano Mei 28, 2025 ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa mikakati ya Jeshi la Polisi kupitia dhana Polisi Jamii katika kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuzuia na kupambana na vitendo vya uhalifu vinavyohusishwa na matumizi mabaya ya teknolojia.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Chuo hicho, Dkt Grace Benedict, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuona umuhimu wa kuwafikia wanafunzi kwa elimu hiyo, akibainisha kuwa ni muda muafaka kwani vijana wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii isivyofaa na kujikuta wakikumbana na matatizo ya kisheria au kijamii.
Ameomba elimu hiyo iwe endelevu ili kusaidia kujenga kizazi cha vijana waadilifu na wenye maarifa chanya ya kidijitali.
Naye, Raisi wa Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo, Jackson Kudoswa amesema kuwa elimu waliyoipata imewafungua macho na itawasaidia wanafunzi wengi kufikia malengo na sasa wako tayari kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya kwa wenzao.
*Kutoka: Dawati la Habari Polisi Mwanza*