Na Dk. Reubeni Lumbagala
SERIKALI kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inawajibika kupokea maombi ya mikopo na kutoa mikopo kwa waombaji waliokidhi vigezo vilivyowekwa. Bodi ya Mikopo ambayo sasa imetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004, hadi Februari 2025, HESLB inajivunia kutoa takribani shilingi trilioni 8.2 kwa waombaji mbalimbali zaidi ya 830,000 ambao sasa si waombaji tena bali ni wanufaika wa mikopo hiyo.
Kiukweli, fedha hizi ni nyingi sana ambazo zimetolewa na serikali kwa nia njema ya kuwasaidia wanafunzi ambao kutokana na hali za kiuchumi wao na familia zao hawawezi kugharamia gharama za elimu ya juu, hivyo kuhitaji kuwezeshwa raslimalifedha ili kumudu kulipa ada, malazi, kununua chakula, vitabu, kuhudhuria mafunzo kwa vitendo na masuala mengineyo.
Ni muhimu kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kufahamu kuwa mikopo waliyokopeshwa na serikali kupitia Bodi ya Mikopo inapaswa kurejeshwa pindi wanapohitimu masomo yao hasa baada ya kuwa na kipato ili kuwawezesha waombaji wengine kunufaika nayo.
Takwimu zilizotolewa Okotba mwaka juzi 2023, zilikuwa zinaonesha kwamba shilingi trilioni 1.34 kati ya shilingi trilioni 2.1 zinazodaiwa, sawa na asilimia 64 zilikuwa zimekusanywa na bado wakati huo kulikuwa na kiasi cha shilingi bilioni 758 ambacho kilikuwa hakijarejeshwa, licha ya wanufaika wengi kuwa na uwezo wa kulipa.
Wigo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi unaweza kuongezeka endapo wanufaika waliohitimu masomo yao watarejesha mikopo hiyo kwa wakati baada ya kuanza kuingiza kipato kwa kuajiriwa au kujiajiri. Bila marejesho mazuri kutoka kwa wanufaika, waombaji wengi watakosa mikopo na mwisho watashindwa kuendelea na elimu ya juu.
Kwamba, ni muhimu kwa wanufaika wahitimu wenye kipato yaani walioajiriwa au kujiajiri wenyewe kurejesha mikopo yao kwa hiari ili kuwa na uendelevu mzuri wa utoaji mikopo kwa kuzingatia kuwa kila mwaka kuna ongezeko kubwa la waombaji wa mikopo ambao wana sifa za kukopesheka na ambao kupitia marejesho ya wanufaika pamoja na fedha zinazotolewa na serikali, Bodi ya Mikopo itaweza kuwakopesha waombaji wengi zaidi.
Waajiri wanao wajibu wa kuwasilisha taarifa za wafanyakazi wao wenye elimu ngazi ya stashahada au shahada ili Bodi ya Mikopo iweze kujiridhisha kama wafanyakazi hao ni wanufaika wa mikopo au la. Na endapo itathibitika kuwa mfanyakazi ni mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu, mwajiri atapaswa kukata asilimia 15 ya mshahara wa mfanyakazi mnufaika wa mkopo wa elimu ya juu kila mwezi na kuwasilisha makato hayo Bodi ya Mikopo hadi pale mfanyakazi mnufaika atakapomaliza deni lake lote.
Aidha, kwa waliojiajiri wenyewe kama mamalishe, babalishe, bodaboda, mafundi wa fani mbalimbali, wakulima, wafugaji, wavuvi na wengineo, wanaweza kujisajili kwenye mfumo ili kujua deni lao na kupata Namba Maalumu ya Malipo (Control number) ambayo wataweza kulipa kiasi fulani cha fedha kulingana na kipato wanachoingiza ili mwisho wa siku waweze kumaliza deni lote na kuwawezesha wengine kupata mikopo kama walivyopata wao. Pia, kupitia kujisajili huko kwenye mfumo, wahitimu wanufaika watajua mwenendo wa taarifa za madeni yao.
Kimsingi, utaratibu wa kulipa deni si lazima mnufaika awe ni mfanyakazi wa sekta rasmi yaani aliyeajiriwa. Hapana. Hata aliyejiajiri mwenyewe au asiye katika ajira rasmi anaweza kuanza kulipa deni lake hadi akamaliza kulilipa deni lote. Cha muhimu ni mnufaika mhitimu awe na kipato, na kipato kinaweza kuwa ni kwa kuajiriwa au kujiajiri.
Ni hivi: Lipo kundi kubwa la wanafunzi wanaohitaji kukopeshwa ili kutimiza ndoto zao za kielimu, njia mojawapo ya kuwasaidia wanafunzi hawa ni wanufaika wahitimu kulipa kwa hiari mikopo yao ili nao waweze kukopesheka. Pengine mhitimu mnufaika anaweza kuwa ana kipato lakini hajaanza kurejesha mkopo wake, ni vyema kujifichua na kuanza kulipa kwa hiari. Kwa kufanya hivyo, mhitimu mnufaika atakuwa ameshiriki kutimiza ndoto za kielimu za vijana wengi wanaohitaji kuwezeshwa mkopo, na huu ndiyo uzalendo na moyo wa kupenda maendeleo.
Ni vyema kila mnufaika ajiulize kwamba kama asingepata mkopo ingekuwaje kwake kupata elimu ya juu? Hivyo aone umuhimu wa kuwa sehemu ya kuhakikisha wadogo zake pia wananufaika kupitia yeye kwa kurejesha mkopo wake.
Cha kuzingatia ni kwamba umuhimu wa wanufaika kurejesha mikopo ni mkubwa kwa maendeleo ya elimu ya juu nchini. Mbali ya Fedha zinazorejeshwa kutumika tena kutoa mikopo kwa wanafunzi wengine kama ilivyoelezwa kwa msisitizo hapo awali, kurejesha mikopo kunasaidia kudumisha uadilifu na uwazi katika mfumo wa utoaji mikopo, na kuimarisha imani ya umma katika utendaji wa HESLB.
Kwa ujumla, kurejesha mikopo ni jukumu la kijamii linalosaidia kujenga taifa lenye elimu bora na fursa za maendeleo kwa vizazi vijavyo.
Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni iliyoko wilaya ya Pangani mkoani Tanga.
Maoni: 0620 800 462.