Na Shomari Binda-Tarime
MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Mara Ghati Chomete amefanikisha kuchangisha zaidi ya milioni 10 kwenye harambee ya kikundi cha wanawake wajasiliamali Nyansembe kilichopo Nyamongo.
Harambee hiyo imefanyika jana aprili 27,2025 huku ikihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wanaofanya kazi na kikundi hicho kutoka mgodi wa Barrick North Mara.
Akizungumza na wana kikundi hao Mara baada ya kufanikisha kiasi hicho cha fedha amesema kiende kiwasaidie sehemu ya malengo yao waliyoyakusudia.
Amesema ili kufikia malengo waliyoyakusudia wanapaswa kushirikiana zaidi na kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea kipato.
Ghati amesema kwa kuwa lengo la kukusanya milioni 30 halikuweza kutimia wanapaswa kuandaa harambee nyingine na kuwaalika watu mbalimbali ili waweze kuwachangia.
" Niwapongeze kwa hiki ambacho kimepatikana leo kwa malengo yenu mliyoyakusudia mnapaswa kuandaa harambee nyingine.
" Lakini hiki ambacho kimepatikana leo kiende kikaongeze nguvu kwenye kazi zenu na naamini kitatatua sehemu ya changamoto mlizozieleza kwenye risala yenu",amesema.
Awali wanawake hao wajasiriamali walieleza kupitia risala yao kuwa wanahitaji mashine ya kukoboa unga, mashine ya unga lishe na Bajaji kama chombo cha usafirishaji wa mazao yao kutoka stoo kwenda mgodini.
Mbungo huyo alichangia fedha taslimu shillingi millioni mbili 2,000,000/= diwani wa Kata ya Matongo (Nyamongo) Mhe.Godfrey Mwita Kegoye akichangia fedha taslimu shilingi milioni 1,000,000/= kampuni ya RIN COM LTD ikichangia fedha taslimu laki tano 5,000,000/= pamoja na wanakikundi na waalikwa wengine.