Wananchi wa Kata ya Bwiregi wamempongeza Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini kwa kufanikisha Bilioni 1.5 ambayo ilitumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza kwenye mkutano na wajumbe wa CCM na wananchi katika Ziara ya Mbunge kwenye Vijiji vya Kitasakwa, Ryamisanga, Kamgendi na Masurura Diwani wa Kata ya Bwiregi Nyagheti Adam amesema kuwa ni muda wa kumpongeza mbunge kwa yale mema aliyofanya kwenye kata hiyo.
"Wananchi hawa wameazimia kuwa Mhe. Sagini upewe maua yako uliahidi na ukaleta fedha nami nikawa kiungo muhimu katika kusukuma maendeleo hivyo naamini utarudi tena kwenye ubunge sioni kitu kinachokwamisha, niwaombe watu msirithi uadui wa mtu na ogopeni matapeli wanaokuja kukuambia Sagini na Nyagheti wamefanya nini wewe muulize pia amefanya nini," amesema Diwani Nyagheti.
Naye Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amewashukuru wananchi na kuwaomba kuendelea kumuamini na kumpa ushirikiano huku akiwahidi kumalizia viporo ambavyo vimebakia.
Pia Mhe. Sagini amesema kuwa miradi ya maendeleo yote iliyofanyika katika Kata ya Bwiregi ni kwa ajili ya mafiga matatu muunganiko wa Rais, Mbunge na Diwani wote wanatokana na CCM huku akitaja baadhi ya miradi kuwa ni maji safi na salama kwenye vijiji vyote Kitasakwa, Ryamisanga, Kamgendi na Masurura, Kwenye Shule ya Sekondari ya Bumaswa wamefanikisha ujenzi wa Bweni, Vyoo, Madarasa mapya, Tanki la Maji ambapo wanatarajia kupokea wananafunzi wa Kidato cha Tano mwaka huu.
Aidha Mhe. Sagini amesema kuwa maendeleo yaliyofanyika Butiama ni kwa sababu ukarimu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa usikivu wake mpaka kutoa zaidi ya bilioni 102 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha MJNUAT, Jengo la Halmshauri Wilaya, Hospitali ya Wilaya, Vituo vya Afya Vitano, Chuo cha VETA, Shule za Sekondari mpya 10, Shule ya Ufundi ya Amari nk.