Angola Yajiondoa Upatanishi Mgogoro wa Mashariki Mwa Drc

GEORGE MARATO TV
0


 Rais wa Angola, Joao Lourenço aliteuliwa kuwa mpatanishi na AU mwaka 2022 katika jaribio la kumaliza mzozo unaohusisha M23 ambao ulizidisha mashambulizi yake mwezi Januari na kunyakua maeneo makubwa ya ardhi katika eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC.

Rwanda inakanusha kuwapa M23 msaada wa kijeshi. Utawala wa Rais Paul Kagame unasema unakabiliwa na tishio katika eneo hilo kutoka kwa kundi la FDLR, lililoanzishwa na viongozi wa kabila la Wahutu waliohusika katika mauaji ya kimbari ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994.

"Angola inatambua hitaji la kujiondoa kutoka kwa jukumu la upatanishi wa mzozo huu ... ili kuzingatia kwa kina zaidi vipaumbele vya jumla vilivyowekwa na shirika la bara," ilisema Taarifa ya ofisi ya Rais wa Angola. 

"Angola daima imekuwa ikiamini katika haja ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya DRC na M23," ofisi ya rais iliongeza.

Tangu mwisho wa 2021, usitishaji mapigano na mapatano kadhaa yamekubaliwa kabla ya kuvunjwa. 

Angola, ambayo ilichukua urais wa zamu wa AU miezi miwili iliyopita, ilisema kwamba itafanya kazi na Tume ya AU kutafuta mpatanishi mwingine.


'Mkutano wenye matunda'

Tangazo hilo linakuja chini ya wiki moja baada ya mazungumzo yaliyopangwa kufanyika katika mji mkuu wa Angola, Luanda, kufutwa baada ya M23 kujiondoa kufuatia kuwekewa vikwazo vya EU kwa baadhi ya viongozi wake wakuu.

Ikirejelea mazungumzo yaliyofutwa ya Luanda, ofisi ya Rais wa Angola ilisema mazungumzo hayo yamekatizwa "kutokana na mchanganyiko wa mambo, ikiwa ni pamoja na baadhi ya mambo ya nje yasiyohusiana na mchakato unaoendelea wa Afrika".

Siku ambayo mkutano wa usuluhishi ulipangwa kufanyika mjini Luanda, serikali ya Qatar ilitangaza kuwa imemkaribisha Rais Kagame wa Rwanda na mwenzake wa Kongo, Felix Tshisekedi, kwa mazungumzo.

Baada ya mkutano huo, maafisa wa Qatar walitoa taarifa,Iliyosema marais hao walithibitisha ahadi yao ya kusitisha mapigano mara moja na bila masharti kama ilivyokubaliwa katika mkutano wa kilele wa Afrika mwezi Februari.

"Mkutano huo wenye matunda ulisaidia kujenga imani katika kujitolea kwa pamoja kwa mustakabali ulio salama na dhabiti wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kanda," iliongeza taarifa hiyo.

Licha ya majaribio ya hivi majuzi ya kusuluhisha usitishaji mapigano, M23 wiki iliyopita walichukua udhibiti wa kitovu cha uchimbaji madini cha Walikale, eneo la mbali zaidi la magharibi ambalo kundi hilo limeingia ndani ya DRC tangu 2012.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top