Serikali imeelekeza kuwa January 27 na January 28, 2025 Watumishi wa Umma katika Mkoa wa Dar es Salaam wafanyie kazi nyumbani isipokuwa wale ambao mazingira yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vya kazi kama vile Watumishi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,Sekta ya Afya na Sekta ya Usafiri na Usafirishaji ili kuepusha usumbufu.
Hatua hiyo inatokana na kufungwa kwa baadhi ya barabara kutokana na ugeni mkubwa wa Watu wanaokuja kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati utakaofanyika Jijini Dar es salaam kesho na keshokutwa.
Taarifa iliyotolewa leo January 26,2025 na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka imesema Benki hazitafungwa na biashara katika Soko la Kariakoo zitendelea kufanyika lakini pia Hoteli na migahawa nayo haitafungwa.
Serikali imewashauri Waajiri katika Sekta binafsi kuruhusu Watumishi wao katika Mkoa wa Dar es Salaam kufanyia kazi nyumbani au kuweka utaratibu ambao hautasababisha changamoto ya usafiri kutokana na kufungwa kwa barabara hizo.
Mkutano huo unaandaliwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika ambapo Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Marais wa Nchi za Afrika 24, Wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika 21, Wakuu wa Taasisi za Kimataifa sita wakiwemo Rais wa Benki ya Dunia, Rais wa Benki ya Afrika na Rais wa Taasisi ya Rockefeller na Washirika wa Maendeleo watano watashiriki Mkutano huo na pia jumla ya Washiriki wengine 2,600 wa ndani na nje ya Tanzania wamejisajili kwa ajili ya mkutano huo.

