Waziri Gwajima apongeza Mchango wa Shirika la Kivulini katika Mapambano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia

GEORGE MARATO TV
0


 Serikali imepongeza Mchango wa shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la Kivulini katika
kuinua uchumi wa kaya na kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,mimba pamoja na ndoa za utotoni.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Dkt.Dororthy Gwajima wakati wa ziara yake katika ofisi za shirika hilo zilizoko nyamhongolo Jijini Mwanza.


Akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa shirika la Kivulini,Dkt.Gwajima ameahidi kuwa serikali itaendelea kuunga mkono shirika hilo ikiwemo kuhakikisha linapata ufadhili zaidi ili kuongeza ufanisi kwenye shughuli za kupambana na ukatili wa kijinsia pamoja na kuinua uchumi wa kaya.

‘’Kivulini wanafanya kazi kubwa ambayo haijasimuliwa vizuri make sio watu wa kupiga kelele,Niseme natambua kwa ukubwa kazi mnayofanya,ushirikiano wenu,Tuna Jukumu moja tu la Kuisemea Kivulini ili isikike na iendelee kupata ufadhili kwa sababu kazi zake ziko kwenye Jamii huko na ni kati ya mashirika yanayofanya kazi vizuri nchini,Niwatie moyo,Kazi ya kucheza na Jamii sio kazi ndogo’’alisema Waziri Gwajima. 


Waziri Gwajima pia amevutiwa na Mbinu bunifu ya sasa inayotumiwa na shirika hilo kutokana na mbinu hiyo kuwezesha Jamii kujenga nyumba za kisasa kwa gharama nafuu katika wilaya za Magu na Misungwi Mkoani Mwanza.

‘’Nilipokuwa waziri wa afya nilienda kuona kivulini Mmejenga nyumba kwa gharama nafuu huku huku Mwanza,Nikaenda nikazindua baadhi,kweli nilibarikiwa sana na hilo Jambo,Laiti teknolojia hii inayotumika Kupitia shirika la kivulini ikafahamika na wengine wakafanya tusingekuwa na nyumba zenye hali mbaya kwenye Jamii zetu,lakini kazi hii haijasemwa vizuri kwa ukubwa wake,Natamani siku moja itafutwe Mkakati wa kuelezea kazi za kivulini pia nilienda kwenye kazi ya mpango wa ujenzi wa masoko ambapo ndani yake kuna sehemu ya kunyonyeshea sokoni kule mwanza nikawaona Kivulini,Nikasema mbona haya mambo hayasemwi,yatasimuliwa na nani?alihoji Waziri Gwajima.





Aidha ameeleza kuguswa na ushirikishwaji wa mashabiki wa Timu za soka za Simba na Yanga katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

‘’Mashabiki wa Mpira wa Miguu Timu za Simba na Yanga wabebe ajenda za kupambana ukatili hapo ndo nilichoka kabisaa na niliona mwitikio mkubwa kwamba unapogusa michezo,Mwitikio unakuwa ni mkubwa,ukiwaelezea na dhana ya uhitaji wa kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto basi ujue Jamii iliyoko pale moja kwa moja imemalizana na lile tatizo’’alisema Dkt.Gwajima




Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kivulini Yassin Ally amemshukuru waziri Gwajima kwa kutenga muda na kufika kwenye ofisi za shirika hilo.


Yasin amesema kuwa ujio wa waziri huyo umewatia moyo na ari ya kuona kwamba serikali inatambua na kuthamini shughuli zinazofanywa na shirika hilo.

‘’Dhamira ya Kivulini ni kuchangia utekelezaji wa vipaumbele na sera za serikali na tumekuwa tukichangia utekelezaji wa mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto na Waziri amefika kwenye shughuli zetu katika mikoa mbalimbali na kujionea lakini leo kwetu Kivulini ni faraja na heshima kubwa ambayo itatupa ari kubwa ya kuendelea kuchangia Jitihada za serikali za kuwaletea watu maendeleo na tunajua eneo hili la ukatili dhidi ya wanawake na watoto linakwamisha Jitihada hizo’’alisema Yassin  




















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top