Ukaguzi wa Magari ya Kubeba Wanafunzi Wang'oa Nanga Mwanza

GEORGE MARATO TV
0


Na Kutoka Dawati la Habari Polisi Mwanza

Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limezindua zoezi la ukaguzi wa magari ambapo limeanza na ukaguzi wa magari yanayobeba wanafunzi wa shule kabla ya mhula wa masomo kuanza na baadaye kukagua magari ya abiria na mizigo.

Uzinduzi wa ukaguzi huo umefanyika leo Disemba 14, 2024 katika kituo kikuu cha mabasi ya mikoani Nyamhongoro kilichopo Wilaya ya Ilemela Jijini humo. 

Lengo la ukaguzi huo ni kuhakikisha vyombo vyote vya moto vinavyotumika katika barabara za umma vinakuwa na ubora kwa matumizi ya umma na kubaini magari yasiyokidhi vigezo kisheria ikiwa ni mkakati wa kuzuia ajali zitokanazo na ubovu wa magari hayo.

Akizungumza na wamiliki wa shule, wasimamizi wa sheria, madereva na wadau wa usafirishaji mkoa wa Mwanza; Mkuu wa Operesheni mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Aloyce Nyantora kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza amesema zoezi hilo ni la hiari kwa sasa na amewataka wamiliki kupeleka magari yao kukaguliwa kabla ya shule kufunguliwa ambapo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wamiliki watakaokaidi kupeleka magari yao kukaguliwa baada ya shule kufunguliwa.

Aidha, ACP Nyantora amewaonya madereva kujiepusha na migogoro na wasimamizi wa sheria kwa kujaza watoto wa shule kwenye gari zaidi ya uwezo wa Gari sambamba na kufuata sheria za usalama barabarani.

Naye Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Mwanza Mrakibu wa Polisi (SP) Sunday Ibrahim na timu yake ameahidi kusimamia zoezi hilo kikamilifu ambalo limepangwa kufanyika kwenye vituo vya Polisi vya wilaya na kwa wilaya ya Nyamagana na Ilemela zoezi litaendelea katika kituo cha mabasi Nyamhongolo.

Sambamba na hayo, Afisa Elimu mkoa wa Mwanza Martine Nkwabi amewaasa wamiliki wa shule kuacha kutumia magari mabovu kubeba wanafunzi, kuondoa vioo vya giza kwenye magari na kuweka wahudumu waadilifu watakaotoa huduma bora kwa watoto.

Zaidi ya magari 50 yamekaguliwa ambapo 37 yamekutwa ni mazima na magari 15 yamekutwa na hitilafu na wamiliki wametakiwa kuyatengeneza kabla ya kuyaingiza barabarani.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top