Fresha Kinasa, Mara.
MJUMBE wa Baraza Kuu la UWT Taifa Mkoa wa Mara Ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa huo Rhobi Samwelly amewahimiza Wananchi wa Wilaya ya Serengeti kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao bila kufanya makosa kwa kuwapigia kura Wagombea wa Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024.
Ameyasema hayo Novemba 26, 2024 wakati wa kuhitimishwa kwa kampeni za kuwanadi wagombea wa nafasi za Uenyekiti wa Vitongoji vya kata ya Stendi Kuu zilizofanyika katika Kitongoji cha Bomani Wilayani humo.
Amesema, maendeleo ya kweli yanafanywa na chama Cha Mapinduzi kupitia Viongozi wake wakitekeleza ilani ya chama hicho ambayo inagusa kila sekta. Hivyo Wananchi watimize wajibu wao wa Kuwachagua Viongozi wa chama hicho kusudi waendelee kuleta maendeleo katika maeneo yao.
"Kesho tunapiga kura mjitokeze kwa wingi sana, niwaombe Wananchi wote msifanye makosa, chagueni wagombea wa chama cha Mapinduzi kwani wao ndio wataleta maendeleo ya kweli katika maeneo yenu. Mabadiliko mnayoyaona Katika sekta ya elimu, maji, afya na huduma nyingine yamefanywa na CCM endeleeni kukiamini chama cha Mapinduzi mwapigie kura Wagombea wake kwa kishindo."amesema Rhobi.
Ameongeza kuwa, iwapo Wananchi watawachagua viongozi wa chama hicho wataweza kuzungumza kwa lugha moja katika vikao vya maendeleo ya kata na Diwani ambaye ni wa chama cha Mapinduzi katika kuhakikisha Maendeleo yanazidi kufanyika kwa kiwango stahiki.
Naye Diwani wa Kata hiyo Mwita Mapancha amesema, wakati anaingia madarakani mwaka 2020 Wananchi wa kata ya Uwanja wa ndege hawakuwa na huduma ya maji na umeme lakini huduma hizo zimeimarika. Na changamoto ndogo ndogo zilizopo zitaendelea kutatuliwa.
Naye Mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Kitongoji cha Bomani Jonathan Marwa amesema, iwapo atachaguliwa atahakikisha fursa zilizopo katika Kitongoji hicho zinatumika vyema kwa ajili ya Wananchi, kuimarisha hali ya ulinzi na usalama na kutenda haki kwa Wananchi wote katika utoaji wa huduma.
"Kesi ndogo ndogo nitahakikisha tunazimaliza wenyewe kwa wenyewe katika Kitongoji chetu siyo kukimbilia polisi kwa kesi ndogo ndogo ambazo tunazimudu. Na pia tutahakikisha tunajenga umoja na kuimarisha usalama katika Kitongoji cherubs."amesema Marwa.
Katibu Mwenezi wa chama cha Mapinduzi Wilaya hiyo Robert Chacha amesema Uongozi haufanyiwi majaribio hata kidogo, hivyo Wananchi wafanye maamuzi sahihi ya kuchagua Viongozi wa serikali za mitaa kutokana na chama hicho.
''Wilaya ya Serengeti tuna Vijiji 78, Chama cha Mapinduzi tumepita bila kupingwa Vijiji 69, ni Vijiji 9 tu ndivyo tunachuana na wapinzani na tumejipanga vyema kushinda kwa kishindo hivyo tisa ili tushinde Vijiji vyote 78 kwa asilimia 100."amesema Chacha.