Na. Aron Msigwa Songea, Ruvuma.
Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama amesema kiwango cha ushamiri wa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI nchini Tanzania kimepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2003/2004 mpaka asilimia 4.4 mwaka 2022/23 kufuatia juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali na wadau wa Sekta binafsi.
Mhe. Mhagama ameyasema hayo leo Novemba 29,2024 mjini Songea, Ruvuma wakati akifungua kongamano la kitaifa la kisayansi na uzinduzi wa usambazaji wa ripoti ya utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2022/23 ambapo amesema kiwango cha maambukizi pia kimepungua kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto kutoka asilimia 18 za mwaka 2010 hadi asilimia 8.1 mwaka 2023 hali inayoongeza usalama wa watoto.
Leo tunazindua usambazaji wa ripoti ya matokeo ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI mwaka 2022 - 2023 katika Kongamano lililohusisha wadau kutoka maeneo mbalimbali nchini. Takwimu hizi zitasaidia makundi mbalimbali katika kupanga mipango ya maendeleo Amesema Mhe. Mhagama.
Ameongeza kuwa ripoti ya utafiti iliyozinduliwa inaiwezesha Serikali kufahamu hali halisi ya kiwango cha maambukizi ya VVU pia kuonesha mafanikio, changamoto na mikakati inayopaswa kuchukuliwa katika mapambano dhidi ya VVU huku akiipongeza Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na Baraza la Watu wanaoishi na VVU nchini Tanzania (NACOPHA) kwa kuweka mikakati imara , kuishauri Serikali na kuwaelimisha Watanzania kuhusu mapambano dhidi ya VVU.
Natoa wito kwa viongozi wenzangu na watu wenye uwezo wa kusambaza taarifa hizi wakiwemo wanamichezo, viongozi wa dini, wanasiasa, waandishi wa habari washiriki kikamilifu katika usambazaji wa takwimu hizi
Amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI kwa kuimarisha huduma za afya nchini hali iliyochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi ya VVU.
Natoa wito kwa kila Mtanzania kuwa mlinzi wa mafanikio ya mapambano hayo hapa nchini ili kuongeza ufanisi wa mapambano dhidi ya hali zote za unyanyapaa. Wizara tumetenga fedha kwa ajili ya kuanzisha kituo cha pamoja dhidi ya mapambano ya VVU, uanzishwaji wa miongozo na kusisitiza uzingatiaji wa mila na desturi nzuri za unasihi katika maeneo ya utoaji wa elimu katika maeneo mbalimbali nchini
Katika hatua nyingine ametoa wito kwa TACAIDS , wadau wa sekta ya umma na binafsi waendelee kuwekeza katika Sekta ya afya katika uanzishaji wa viwanda vya uzalishaji bidhaa, vifaa tiba na dawa zinazohusiana na udhibiti wa UKIMWI na VVU ndani ya nchi.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutoa hamasa ya utoaji wa huduma za msingi kwa kuongezea nguvu zaidi katika kuyafikia makundi yaliyo katika hatari ya maambukizi ya VVU yakiwemo makundi ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, madereva wa malori ya masafa marefu, wachimbaji wa madini migodini, wavuvi, wafanyakazi wa mashamba makubwa na kutoa wito kwa akina Baba wawe na hamasa ya kwenda kupima VVU ili kuongeza ushiriki wao katika mapambano dhidi ya VVU nchini.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya kudhibiti Tanzania (TACAIDS) Dkt. Jerome Kamwela ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Ruvuma kwa kukubali kuwa mwenyeji wa kongamano hilo na tukio la uzinduzi wa usambazaji wa ripoti ya utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2022/23 ambapo amesema utafiti huo ulifanyika kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea na hufanyika kila baada ya miaka 5.
Tumelenga kumaliza janga la UKIMWI mwaka 2030. TACAIDS tumepanga kusambaza matokeo ya utafiti huu kwenye ngazi ya Miko ana Wilaya ili kuwezesha wadau mbalimbali kupata taarifa za utafiti huo na kuchukua hatua na kuongeza juhudi za kupambana na maambukizi mapya ya VVU pia kuweka mikakati katika maeneo ambayo bado yana changamoto.
Amesisitiza kuwa TACAIDS kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya VVU na UKIMWI imeandaa mpango endelevu wa mwitikio wa VVU na UKIMWI unaolenga kuongeza mikakati ya uendelevu ambayo Tanzania itatekeleza mpango wa kupunguza maambukizi mapya ya VVU na vifo vinavyotokana na UKIMWI kwa asilimia 95, kupunguza unyanyapaa na ubaguzi hadi chini ya asilimia 5.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Salum Kassim Ali Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo ameeleza kuwa matumizi ya takwimu rasmi ni muhimu katika kuchochea maendeleo nchini, kuongeza uwajibikaji, kuleta mabadiliko na matokeo chanya yaliyokusudiwa katika mipango yote ya maendeleo.
Amesema takwimu rasmi zinazotokana na utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI za mwaka 2022 -2023 zitaiwezesha Tanzania kujipima na kutathmini ufanisi wa mbinu za kukabiliana na maambukizi mapya ya VVU akisisitza kuwa takwimu zilizokusanywa zimezingatia vigezo vyote na zitasaidia kupanga mipango ya ndani na kutumiwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania.
Nawaomba watumiaji wa takwimu hizi wasipotoshe, wazitumie kwa usahihi na sio kwa lengo la kupotosha au kujipatia umaarufu kwa kuwa yanalindwa na Sheria amesema Salum Kassim Ali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Programu, CDC Dkt. George Mgomella Akizungumza kwa niaba Balozi wa Marekani nchini Tanzania ameeleza kuwa Tanzania imeendela kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya VVU kupitia programu mbalimbali ambazo zimesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza madhara kwa watu wanaoishi na VVU na maambukizi mapya ya VVU.
Amesema matokeo ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI kwa mwaka 2022 - 2023 yanaonesha kuwa utoaji wa huduma kwa wanaoishi na VVU na uzuiaji wa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua umeimarika nchini Tanzania.
Utafiti huu unatupa kazi ya kuongeza nguvu zaidi katika eneo la kukabiliana na maambukizi mapya husani kwa kundi la vijana kuanzia Miaka 15 amabao wanaonekana kuchangia maambukizi mapya. Serikali ya Tanzania imejitahidi kuimarisha huduma za afya, kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha huduma Kinga na matibabu kwa wananchi
Akizungumza kwa niaba ya Baraza la Watu Wanaoishi na VVU Tanzania (NACOPHA), Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza hilo, Deogratius Rutata ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia kwa kuendelea kuijali jamii ya watu wanaoishi na VVU Tanzania kwa kuipatia dawa za kufubaza VVU
Tunaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuimarisha utoaji wa taarifa zikiwemo takwimu za kuhusu maambukizi ya VVU na UKIMWI hapa nchini kwa mwaka 2022-2023 .Hatua hii inatuongezea jukumu la kuongeza mapambano zaidi ya kufikia maambukizi sifuri ifikapo 2030.
NACOPHA tutaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa Afua za UKIMWI kuunga mkono mapambano dhidi ya maambukizi VVU kwa kuwa tunalo jukumu muhimu la kuisaidia Serikali na jamii nzima kupata matokeo chanya.