Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza Mhe.Johari Samizi amewongoza wakazi wa Wilaya hiyo katika uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Vijiji na Vitongoji.
Mhe, Samizi amepiga kura katika Kituo cha kupigia kura kilichopo ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Misungwi Kitongoji cha Misungwi D Kijiji cha Misungwi na kuwahimiza Wananchi kujitokeza kupiga kura mapema na kutimiza haki ya Msingi na ya kikatiba ya kuwachagua Viongozi.
Amewasihi kuendelea na utulivu na Amani wakati wote wa zoezi la upigaji kura na kusubiri matokeo yatakapotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Misungwi.
Bi. Semeni Juma na Chausiku Mujima wakazi wa Kijiji cha Misungwi ni miongoni mwa Wananchi waliopiga kura mapema Leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi pamoja na mvua kunyesha wamefurahi kutumia haki ya kikatiba ya kuwachagua Viongozi wa Kijiji na Kitongoji na kuhakikisha wametumia Fursa ya kuchagua Viongozi Bora na wabunifu na wanaowataka.
Kwa upande wao,Watu wenye ulemavu wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wameiomba serikali kuwawekea mazingira wezeshi ya kupiga kura kwa kuwawekea karatasi zenye maandishi ya nukta nundu yatakayowawezesha kupiga kura bila kusaidiwa na mtu yeyote
Wamesema kutokana na zoezi la upigaji kura kuwa la siri kwa mtu anayetaka kuwachagua viongozi awapendao hivyo wakiwekewa karatasi zenye maandishi hayo yatawasaidia kuwapigia kura viongozi wanaowataka
Naye Diwani wa kata ya Usagara ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya Misungwi Kashinje Machibya amesema hoja hiyo ni ya msingi hivyo kuahidi kulifikisha suala hilo kwenye ngazi husika