Naibu wa rais nchini Kenya Rigathi Gachagua amesema kwamba atawasili bungeni hapo kesho ili kujitetea.
Naibu huyo ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kumuondoa madarakani amesema kuwa atawasili mbele ya bunge pamoja na kundi lake la mawakili mwendo wa saa kumi na moja ili kujitetea.
Akizungumza na waandishi habari nyumbani kwake huko Karen Jijini Nairobi, Kiongozi huyo amesema kwamba kabla ya yeye kuwasilisha hoja yake ya kujitetea atahitaji bunge kusikiliza maoni ya Wakenya waliomchagua.
Kiongozi huyo alisema anatumai wabunge watamruhusu kujibu tuhuma zote bila kuingiliwa.
Gachagua, amesema aliita kikao hicho na waandishi wa habari kutoa utetezi wake kwa Wakenya waliomchagua kabla ya kuwasili mbele ya wawakilishi hao.
"Nafikiri ni haki wakati wabunge wataamua kwamba wanataka kumwondoa Naibu Rais afisini, watu waliomchagua Rigathi Gachagua kuwa Naibu Rais wasikie upande wake," akasema.
Hoja ya kuondolewa mashtaka iliwasilishwa Septemba 26 na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Mbunge huyo alitaja sababu 11 ambazo anataka Gachagua aondolewe afisini, ikiwa ni pamoja na kujilimbikizia mali ya hadi Sh5.2 bilioni katika muda wa miaka miwili pekee, kumhujumu Rais na kukuza ukabila.
Aidha amepuuzilia mbali mchakato wa kusikilizwa kwa maoni ya Wakenya kuhusu kuondolewa kwake madarakani akisema kwamba mpango wote huo ulishindwa kuafikia malengo yake.
“Majibu ya Naibu Rais hayakuwapo ili kuwawezesha kufanya uamuzi sahihi,” Gachagua alisema na kuongeza kuwa mchakato huo ulifanywa katika njia ambayo Wakenya wengi hawakuweza kufahamu.
Akiangazia baadhi ya mashtaka yaliowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mutuse Mwengi ambapo ni pamoja na masuala ya Ufisadi, kiongozi huyo amesema kwamba baadhi ya mali anazomiliki ni urithi kutoka kwa ndugu yake mkubwa aliyefariki.
Gachagua anasema kuwa sehemu kubwa ya utajiri wake wa Sh5.2 bilioni ni sehemu ya mali ya ndugu yake marehemu Nderitu Gachagua.
'Heshimuni mtu aliyekufa', Gachagua alimwambia mbunge aliyewasilisha hoja ya kutaka aondoke madarakani bungeni.
Kiongozi huyo anasema kwamba Nderitu aliwakabidhi yeye pamoja na wakili mkuu Njoroge Regeru, na Mwai Mathenge mali yake ya kidunia ambayo ilikuwa igawanywe kwa familia yake.
Gachagua amekanusha madai hayo yote na kuyataja kuwa ni uwindaji unaochochewa kisiasa.