Mhe Esther Matiko Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara na Mkurugenzi wa taasisi ya Matiko Foundation ameendelea na ziara yake ndani ya Wilaya ya Tarime kwa kuzitembelea Shule za Sekondari Nkende na Rebu zinazopatikana ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime na kufanya mazungumzo na Walimu na Wanafunzi wa Shule hizo.
Ikiwa ni utendaji wa majukumu yake ya kibunge, Mhe Esther Matiko amezungumza na Walimu hao na kupokea changamoto mbalimbali ambazo atakwenda kuziwasilisha bungeni kwa ajili ya kufanyiwa kazi na serikali kuu.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Nkende Mwl Nchagwa Chacha amemueleza Mhe Esther Matiko changamoto kubwa inayoikabili Shule hiyo ni ukosefu wa Mabweni ya Wanafunzi, jambo lililopelekea Shule hiyo kuanzisha mchakato wa ujenzi kwa kushirikiana na wazazi na wadau wengine wa elimu.
Sambamba na changamoto hiyo Mwl Chacha hakusita kumpongeza Mhe Esther Matiko kwa kutimiza ahadi zake alizoahidi shuleni hapo ikiwa ni pamoja na utoaji wa Taulo za Kike kupitia taasisi ya Matiko Foundation iliyo chini ya Mhe Esther Matiko.
Mhe Matiko amefika shuleni hapo na kutimiza ahadi yake ya kuwapatia TV na King’amuzi walimu wa Shule hiyo vikiwa na thamani ya Tsh 700,000/= kupitia taasisi ya Matiko Foundation.Sambamba na TV hiyo Mhe Esther Matiko amekabidhi mpira wa Miguu na Pete kwa Wanafunzi ikiwa na thamani ya Tsh 200,000
Mhe Esther Matiko amezipokea changamoto zingine za kiutumishi zilizosemwa na Walimu wa Shule hiyo na kuahidi kuzifikisha kwa viongozi wa serikali kwa kupitia vikao vya bunge na hata njia zingine ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Ziara ya Mhe Esther Matiko imeendelea kwa kuitembelea Shule ya Sekondari Rebu na kufanya mazungumzo na Walimu na Wanafunzi wa Shule hiyo.
Akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Rebu Sekondari Mhe Matiko amesema, “Huwa nikipita kwenye mashule nazungumza nanyi nikiwaasa watoto wa kike mjikite kwenye kusoma maisha mengine mtayakuta mbeleni msidanganyike muwambie wawache msome, mnawaheshimu wawaheshimu na nyie wawaache msome mfikie ndoto zenu. Watoto wa kiume pia muache kukuambia kwenye kuendesha Bodaboda na kwenda migodini kufanya vibarua, hivyo Pesa mnavyovipata ni vidogo wekezeni kwenye elimu mtavuna zaidi ya sasa”.
Katika kuendeleza michezo mashuleni Mhe Mbunge Esther Matiko kupitia taasisi yake ya Matiko Foundation amekabidhi vifaa vya michezo kwa Wanafunzi wa Shule hiyo Mpira wa Pete na Miguu na Jezi za mpira wa Pete na Miguu) vikiwa na thamani ya Tsh 700,000/=
Mhe Esther Matiko ameahidi kutoa zawadi ya Mbuzi wawili kwa ajili ya mashindano ya kimadarasa (Interclass Competition) ikiwa ni kuunga juhudi za Shule hiyo kuendeleza michezo mashuleni. Itakumbukwa hii sio mara ya kwanza Mhe Esther Matiko kufadhili mashindano hayo shuleni hapo.
Wakipokea vifaa hivyo vya michezo Mkuu wa Shule ya Rebu amemshukuru na kumpongeza Mhe Matiko kwa jinsi anavyotekeleza ahadi zake kwa wakati pasipo kuchelewa na amekuwa nao bega kwa bega pale wanapomuhitaji. Itakumbukwa Mhe Esther Matiko aliipatia Shule hiyo Projector na Computer zinazotumika kwenye ufundishaji shuleni hapo
Walimu wa Shule hizo na Wanafunzi wote kwa pamoja wameipongeza taasisi ya Matiko Foundation na kusema imekuja wakati muafaka ili kusaidia mambo mambo mbalimbali yanayohusu idara ya elimu kwa watu wa Tarime na Tanzania kwa ujumla