Maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha vijana kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) yameanza kuzaa matunda baada ya vijana wa BBT Uvuvi waliowezeshwa kufuga samaki kwenye vizimba jijini Mwanza kuanza kuvuna samaki wao.
Hayo yamebainika wakati Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliposhiriki zoezi la awamu ya kwanza la uvunaji wa samaki aina ya Sato lililofanywa na Kikundi cha Vijana cha TWIHAME kinachofanya shughuli zake za ufugaji wa samaki kwa njia ya Vizimba katika eneo la Kisoko, Kata ya Luchelele, wilayani Nyamagana, jijini Mwanza.
Akizungumza baada ya kushiriki zoezi hilo la uvunaji, Waziri Ulega amemshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia kwa kutoa takriban bilioni 2.2 na kuviwezesha vikundi 11 vya vijana kufanya ufugaji wa samaki katika eneo la Kisoko ambapo vijana hao wameweza kuwekeza vizimba zaidi ya 100 katika eneo hilo.
“Leo katika kizimba hiki kimoja tu ambacho watavuna samaki takriban 4000, vijana hawa watapata kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 30, inaleta matumaini makubwa sana, na muitikio wa uwekezaji katika ziwa victoria kupitia vizimba ni mkubwa sana, muitikio huo utasaidia kupunguza masuala ya uvuvi haramu kwa sababu wavuvi wanakwenda kuwa na kazi mbadala”, amesema
Mmoja wa wanufaika wa Vizimba, ambaye pia ni Katibu wa Wanufaika, Wilaya ya Nyamagana, Bw. Omary Mangu amemshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa kuwawezesha mkopo ambao hauna riba ili waweze kufanya shughuli za kufuga samaki ambapo matunda ya mkopo huo wameanza kuyaona.
Septemba 25, 2024, Vijana wa Kikundi kingine kinachojulikana kwa jina la Nguvu Kazi walianza kuvuna tani 13.37 kutoka katika vizimba 6 na baada ya kuwauza walifanikiwa kupata kiasi cha shilingi zaidi ya Milioni 100.
Itakumbukwa kuwa, Januari 30 mwaka huu, akiwa jijini Mwanza, Mhe. Rais Samia alizindua mradi wa vizimba 222 na Boti 160 kwa ajili ya kuwakopesha wavuvi nchi nzima ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija na kuboresha kipato chao.