Mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania(TPA)imeanza rasmi kusimamia shughuli za utendaji kazi wa kibandari katika mwalo wa kirumba Jijini Mwanza ambayo awali ilikuwa ikisimamiwa na halmashauri ya manispaa ya ilemela.
Meneja wa bandari kanda ya ziwa victoria Erasto Lugenge amesema kuwa mamlaka hiyo imechukua hatua hiyo ikiwa ni utekelezaji wa tangazo la serikali namba 855 la tarehe 24/12/2023
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Mwanza,Lugenge ametaja baadhi ya shughuli zitakazopewa kipaumbele na Tpa kuwa ni pamoja na kudhibiti shughuli za usalama wa vyombo vyote vya majini vinavyoegesha kwenye mwalo huo ili kuhakikisha kuwa abiria na mizigo inayosafirishwa inakuwa salama.
Mipango ya baadaye ya mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania ni kujenga miundombinu ya kisasa pamoja na kusimamia shughuli za upakuaji na upakiaji wa shehena katika mwalo huo pamoja na mialo mingine iliyorasimishwa kupitia tangazo hilo.
“Napenda kuchukua fursa hii kuutarifu umma hususani wakazi wa mji wa mwanza pamoja na mikoa Jirani ambao wanatumia ziwa victoria kwamba kuanzia 12/10/2024,Tpa itaanza rasmi utekelezaji wa tangazo hilo la serikali linaloitaka Mamlaka hiyo kusimamia rasmi shughuli za utendaji kazi wa kibandari kwenye mwalo wa mwaloni kirumba”alisema Lugenge na kuongeza kuwa
‘’Faida kubwa ni kuwa sasa vyombo vinavyotoa huduma ya usafiri na usafirishaji vitakuwa vinadhibitiwa rasmi ambapo usalama wa vyombo hivyo utakuwa wa uhakika na tutakuwa tunafahamu abiria wanaondoka na chombo gani na chombo hicho kiko salama au la”
Aidha Meneja Lugenge amewaasa watumiaji wa bandari za ziwa victoria kutumia bandari rasmi kutokana na bandari hizo kuwa na miundombinu kwa ajili ya kutoa huduma huku suala la usalama wa abiria na mali zao linapewa kipaumbele kwenye bandari hizo ikilinganishwa na bandari bubu.
Ziwa victoria upande wa nchini Tanzania lina bandari 358 ambapo kumi tayari ikiwemo mwalo wa kirumba tayari zimerasimishwa huku bandari 348 zilizosalia zikiwa hazijarasimishwa na hivyo kuchangia katika kuhatarisha usalama wa abiria na mali zao pamoja na kutumiwa na wahalifu kupitiza bidhaa haramu sanjari na bandari bubu kutumiwa na baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kodi.