Na Shomari Binda-Musoma
WANAFUNZI 62,214 kutoka Mkoa wa Mara wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi utakaoanza kesho Septemba 11.
Akizungumza na George Marato Tv leo ofisini kwake Katibu Tawala mkoa wa Mara Gerald Kusaya amesema kati ya wanafunzi hao wavulana ni 29,424 na wasichana ni 32,790.
Amesema wanafunzi hao wanatarajiwa kufanya mtihani wa darasa la 7 kwenye shule 876 ambazo zitakuwa ni vituo vya mtihani.
Kusaya amesema wanafunzi hao ni wale walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2018 na wanakamilisha mzunguko wao wa kielimu wa miaka 7 mwaka 2024 na watakuwa kwenye mikondo 2,756
Ameongeza kuwa mwaka huu Baraza la Mitihani Tanzania limefanya maboresho mapya kwa mwaka 2024 tofauti na yaliyofanyika 2013 ambapo mtihani wa kuhitimu darasa la 7 utajibiwa kwenye karatasi za maswali.
Amesema hiyo imetokana na Baraza la Mitihani kufanya mabadiliko ya utunzi wa mitihani kwa kufuata mtindo mpya ( Format) hivyo hakutakuwa na OMR za kujibia.
" Mitihani hii itafanyika kwa siku 2 septemba 11 na 12 na kwa mkoa wa Mara maandalizi yote tayari yamekamilika na mitihani imefika vituo husika.
Kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi tunawatakia wanafunzi wote mtihani mwema kuanzia hapo kesho",amesema.
Aidha Katibu Tawala huyo amewataka wanafunzi na wasimamizi kujiepusha kufanya udanganyifu wowote ili kujiepusha na matatizo ikiwemo kufutiwa matokeo.