Na Mwandishi Wetu, MUHEZA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mh Dk Doto Biteko, amehimiza jamii kudumisha ushirikiano na mahusiano mema kati ya mzazi, mwalimu na mwanafunzi, ili kumjenga mtoto katika ubora wa maisha yake na taaifa kwa ujumla.
Mhe Dk Biteko ameyasema hayo leo Septemba 30, 2024 alipokuwa akizindua kampeni ya Mtoto wa Leo Samia Kesho, ikiwa ni sehemu ya shughuli za Juma la Elimu katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Amesema ushirikiano na mahusiano hayo ni nyenzo muhimu ya kujenga mazingira bora kwa mtoto kuanzia ngazi ya familia, kwenye jumuiya za watu na shuleni anapopata elimu na maarifa ya kumfanya (mtoto) kuwa mwenye manufaa na tija katika ngazi zote.
Mhe Dk Biteko, amewaelekeza walimu kumtazama mtoto kama kiongozi, mhandisi, daktari, mwanataaluma, kiongozi ama mzazi bora wa baadaye, na hivyo kumlinda, kumpa elimu, ujuzi, maarifa na kumlinda dhidi ya dhuluma zinazomkabili.
Pia amewaasa wazazi na walezi kuepuka matumizi majina na maneno yasiyofaa kwa watoto, kwani kwa kufanya hivyo ‘wanawapandikizia’ hulka na tabia zisizoendana na uhalisia wao ili waendelee kutamani kuwa viongozi na wazazi bora wa baadaye.
Amesema, Serikali ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuboresha elimu kama ilivyo kwa sekta nyingine, na kutoa mfano katika kipindi cha takribani miaka mitatu, bajeti ya wizara husika imepanda kutoka Shilingi bilioni 903.9 (2021/2022) hadi kufikia Shilingi trilioni 1.114 (2024/2025).
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amesema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa uboreshaji elimu, baada ya vikao vyake vya Wakuu wa Wilaya hivi karibuni.
Amesema, mazingira bora katika sekta hiyo yamechangia kupanda kwa ufaulu mkoani humo, akitoa mfano katika shule za msingi, umepanda kutoka asilimia 71 mwaka 2022 kufikia asilimia 74 (2023), wakati kwa sekondari ni kutoka asilimia 84 (2022) kufikia asilimia 89 (2023).
Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainab Abdallah aliyeanzisha kampeni hiyo, amesema inalenga kuleta ufanisi katika sekta ya elimu kupitia shughuli kuu za upatikanaji madawati, madarasa na kufuta sifuri na daraja la nne kwa matokeo ya kidato cha nne na sita wilayani humo.
Kesho Oktoba Mosi, 2024, Mhe Dk Biteko, atafungua Shule ya Sekondari Miles & Kimberly White yenye kidato cha tano na sita, iliyojengwa katika kijiji cha Mapatano wilayani Mkinga kwa gharama ya takribani Shilingi bilioni 7 za Kitanzania.
Gharama hizo zinahusisha pia ukarabati wa shule ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne, ambayo awali ilijulikana kama Shule ya Sekondari ya Sekondari Mapatano.
Ujenzi wa shule hiyo yenye michepuo vya Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM), Fizikia, Kemia na Baiolojia (PCB), Kemia, Biolojia na Kilimo (CBA) na Historia, Jiuografia na Lugha (HGL) umefadhiriwa na Wakfu wa Abbott wenye Makao Makuu yake nchini Marekani.
Ujumbe wa Abbott kutoka Marekani na kujumuisha watumishi wake waliopo nchini, umewasili na kujitambulisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian ofisini kwake leo Septemba 30, 2024.
Mhe Dk Biteko yupo mkoani Tanga kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo, alikuwa katika wilaya ya Muheza ambapo amezindua kampeni ya Mtoto wa Leo Samia wa Kesho, iliyoasisiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe Zainab Abdallah, ikiwa na lengo la kuwezesha upatikanaji wa madawati 7,000, ujenzi na ukarabati wa madarasa.