WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imejipanga kuendelea kuiboresha Sekta ya Afya nchini kupitia utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali vitakavyolenga kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi mijini na vijijini.
Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo Mei 11, 2026 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Mapitio ya Bajeti ya mwaka 2025/26 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27.
Amesema Serikali imeweka mkazo katika kuboresha huduma za afya kwa kuimarisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, kuongeza wataalam wa afya, pamoja na kuendeleza matumizi ya teknolojia katika hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
“Serikali itaendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zenye staha na utu kwa kuboresha mazingira ya utoaji huduma, kupunguza muda wa kusubiri matibabu na kuimarisha mifumo ya kushughulikia malalamiko ya wananchi katika vituo vya afya,” amesema Mhe. Mchengerwa.
Katika hatua nyingine, Serikali imeahidi kuendelea kuwasaidia wananchi kupunguza gharama za matibabu kupitia Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, ambapo kaya zenye uhitaji zitaendelea kusajiliwa huku wananchi wengi zaidi wakihamasishwa kujiunga na huduma hiyo muhimu.
Aidha, Serikali imepanga kuongeza uwekezaji katika viwanda vya ndani vya dawa na bidhaa za afya ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu unaimarika na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Mhe. Mchengerwa amesema Serikali pia itaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika Sekta ya Afya kwa kuunganisha mifumo ya taarifa za afya, kupanua huduma za afya mtandao pamoja na matumizi ya akili unde katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katika upande wa huduma za kinga, Serikali imeweka mkazo kwenye mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko, magonjwa yasiyoambukiza pamoja na kuendelea kuimarisha huduma za chanjo nchini ili kulinda afya za wananchi.

