Na Mwandishi Wetu
WANAWAKE watatu wamebahatika kupata fursa ya kupandikiza mimba bure katika kituo cha kupandikiza mimba cha Kairuki Green IVF (KGIVF), Kilichoko Bunju A Mianzini jijini Dar es Salaam.
Walipata fursa hiyo jana jioni wakati wa droo iliyochezeshwa na mgeni rasmi Jokate Mwegelo wakati wa sherehe za siku ya wanawake zilizoandaliwa na Mtandao wa Elimu ya Afya Kairuki (KHEN) jijini Dar es Salaam .
Wanawake hao ni miongoni mwa wanawake zaidi ya 137 wa mikoa mbalimbali walioomba kupata fursa hiyo ya bure lakini katika mchujo uliofanyika walibahatika wanawake hao watatu pekee.
Kwa wastani gharama za kupandikiza mimba kwa Tanzania ni kati ya shilingi milioni 18 mpaka 20.
Mkurugenzi wa KGIVF, Dk Clementina Kairuki alisema waliopata fursa hiyo watahudumiwa bure kuanzia hatua za awali hadi kupandikiza mimba kama sehemu ya kituo hicho kusaidia jamii.
Alisema wameamua kutoa huduma hiyo bure kama sehemu ya kusherehekea siku ya mwanamke duniani kuwapa furaha ya kupata familia wanawake ambao wamekuwa wakitamani kupata familia lakini wanashindwa kutokana na kukosa pesa.
Alisema KGIVF iliona wanawake wengi wamekuwa wakijitokeza kutaka kupandikizwa mimba kwenye kituo hicho lakini asilimia 30 hawawezi kumudu gharama za huduma hiyo.
“Kuna watu wengi wanapata shida wanatukanwa kwenye familia wanaachika kwenye ndoa kwasababu hawajabahatika kupata watoto, tafiti zinaonyesha kuwa kila ndoa sita moja inachangamoto ya kupata watoto ndiyo maana tukaona tutoe fursa hii,” alisema.
Alisema KGIVF imekuwa ikitoa elimu kwa jamii kuhusu ukubwa wa tatizo hilo na namna bora ya kupata suluhu ya kulitatua kwa kupandikiza mimba.
“Tumetambua kuwa kuna watanzania wengi wenye tatizo hili lakini hawana uwezo wa kuja KGIVF kupandikiza mimba kwasababu ya uwezo wa kifedha ndiyo maana tumechagua wanawake watatu tuwape huduma hii bure kama sehemu ya kutoa elimu kwa jamii,” alisema
Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, Jokate Mwegelo alisema Mtandao wa Elimu ya Afya Kairuki (KHEN) ni mfano wa kuigwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutokana na mambo makubwa waliyofanya.
Alisema KHEN imefanya mambo makubwa ikiwemo kuanzisha Kituo cha kupandikiza mimba KGIVF, Kairuki Hospitali, Kiwanda cha kutengeneza dawa kilichoko Kibaha mkoani Pwani, Chuo Kikuu Kairuki na Kampasi ya chuo hicho iliyoko Boko.
“Mimi ni mdau mkubwa sana wa Kairuki, nimekuwa nikiwasemea sana na leo naomba nijirasimishe kuwa balozi wa Kairuki, nitawasemea vizuri popote nitakapokuwa kwasababu nyinyi mmeonyesha mfano wa kuigwa kwenye kusaidia jamii yetu,” alisema Jokate Mwegelo.
“Mimi nitakuwa balozi wa viwango kwasababu nimeona Kairuki ni taasisi ya viwango vya juu sana, siongei haya kumfurahisha mtu hapa nasema hili kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu, katika taasisi zilizoasisiwa na watanzania wenzetu, Kairuki ni taasisi ya mfano Afrika Mashariki na Kati kwasababu imesimama na haitetereki,” alisema
“Wako watu walianzisha biashara hata miaka mitatu haijafika zikafa, lakini leo hii ukizungumzia Kairuki unazungumzia Hospitali, unazungumzia Kairuki Green IVF, unazungumzia kiwanda cha dawa Kibaha, chuo cha Kairuki ambacho kinawanafunzi zaidi ya 2,000 nani kama Kairuki,” alisema.





















