DODOMA.
SERIKALI kupitia Tume ya Madini imedhamiria kuwawezesha vijana kwa kuwapatia Ajira kupitia Sekta ya Madini,kukuza ujuzi wa kisayansi na uwekezaji pamoja na Kutenga maeneo maalum ya wachimbaji wadogo wa madini,kuwapatia leseni na kuwaendeleza.
Dhamira hiyo ya serikali ni Kuifanya Tanzania kuwa kituo cha uuzaji wa madini katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na kuimarisha masoko ya madini na vito ikiwamo Tanzanite kwa kujenga jengo la Tanzanite Exchange Centre (TEC) katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro.
Kauli hiyo ya Serikali imetoleo leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira Mhandisi Hamisi Kamando kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na Fursa za vijana katika sekta ya Madini Kwa mwaka 2025/2026.
Amesema serikali imeshatenga maeneo maalum ya wachimbaji wadogo wa madini.
"Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imependekeza kutenga maeneo 65 maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika mikoa ikiwemo Mtwara, Manyara, Lindi, Morogoro, Dodoma, Tabora, Geita, Shinyanga, Mwanza na Mbeya". Amesema
"Hatua hiyo inalenga kuwapa fursa zaidi vijana kushiriki katika uchimbaji wa madini na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa". Ameongeza
"kupitia Wizara ya Madini pamoja na Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo ya uchimbaji wa madini kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini ili kwa pamoja waweze kufaidika na rasilimali hii ambayo tumejaliwa" Amesema
Kadhalika,Katika eneo la uongezaji thamani wa madini, Mhandisi Kamando amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini inaendelea kusimamia sera na sheria zinazohakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.
"Hadi sasa kuna viwanda saba vya kusafisha madini vinavyofanya kazi nchini na sekta hiyo imezalisha ajira 273, nyingi zikinufaisha vijana, huku madini yenye thamani ya shilingi trilioni 5.802 yakiongezewa thamani ndani ya nchi kati ya Julai na Desemba 2025".Amesema
Aidha, amesema kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (Mining for Better Tomorrow – MBT), Tume ya Madini ilitoa leseni 273 kwa vikundi 183 vya vijana kati ya Julai na Desemba 2025 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Mara, Kagera, Shinyanga, Morogoro, Dodoma na Njombe.
Amesema Vikundi hivyo vinajihusisha na uchimbaji wa dhahabu, shaba, madini ya vito, chumvi na madini ya ujenzi, ambapo hadi Desemba 2025 vijana 2,550 walikuwa wamepata ajira za moja kwa moja kupitia mradi huo.
Sambamba na hayo amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo kwa kutoa leseni 5,983 kati ya Julai na Desemba 2025, sawa na asilimia 71 ya leseni zote zilizotolewa katika kipindi hicho.
"leseni za uchimbaji mdogo hutolewa kwa Watanzania pekee, huku sehemu kubwa ya waombaji wakiwa vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 45". Amesema
Lengo kuu la kuundwa kwa Tume ya Madini ni kuboresha usimamizi na udhibiti wa uzalishaji na biashara ya madini kwa kuhakikisha Sheria, Kanuni na Taratibu zote zinazoongoza shughuli za madini zinafuatwa ipasavyo ili kuongeza Pato la Taifa.







