Umeme Jua Kukuza uchumi wa Bluu Visiwa 120 Ziwa victoria,Tanganyika na Bahari ya Hindi

GEORGE MARATO TV
0


 Naibu Waziri wa Nishati,Salome Makamba amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa kusambaza umeme jua katika kisiwa cha Bezi wilayani Ilemela mkoani Mwanza kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ifikapo Mei 27 mwaka huu. 

Makamba ametoa agizo hilo kisiwani Bezi wakati akizindua mradi wa kusambaza mifumo ya umeme jua visiwani kwa bei ya Ruzuku.

 

 



Ameitaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kumsimamia kikamilifu mkandarasi ili kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuondoa changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme kwenye maeneo ya visiwani. 

 

Mradi huo unalenga kuweka mifumo 20,000 ya umeme jua katika visiwa 120 vilivyoko katika ziwa Tanganyika na Victoria pamoja na Bahari ya Hindi.

 

Gharama za utekelezaji wa Mradi huo ni Shilingi Bilioni nane ambapo Serikali inagharamia ruzuku hadi ya asilimia 75 katika gharama za uunganishaji umeme.

 

"Maeneo ya visiwani na delta yana changamoto  zikiwemo umbali kutoka Gridi ya Taifa, gharama kubwa za usafirishaji wa vifaa na mtawanyiko wa makazi unaoongeza gharama za usambazaji wa nishati ya umeme, ndio maana Serikali imekuja na mpango huu mahsusi wa matumizi ya mifumo ya umeme jua pamoja na gridi ndogo kama suluhisho la haraka la kuwafikia wananchi wa visiwani na maeneo ya pembezoni." amesema Naibu waziri Makamba


Kwa mujibu wa Makamba, hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ili kurahisisha upatikanaji wa umeme katika maeneo ya visiwani ni pamoja na kutoa ruzuku kwa mifumo ya umeme jua ili kuharakisha upatikanaji wa nishati safi, kupunguza utegemezi wa vyanzo visivyo endelevu kama dizeli, na kuhakikisha gharama za nishati zinakuwa nafuu.

 

"Mradi huo niluouzindua una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Bluu, ambao ni moja ya kipaumbele cha Taifa katika maeneo ya pwani na visiwa" alisema na kuongeza kuwa 

 

"Mifumo ya umeme jua inayofungwa itawawezesha wavuvi kuongeza thamani ya samaki na dagaa na hivyo kuongeza mapato ya wananchi pamoja na Taifa, kuimarisha shughuli za ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, kilimo cha mwani, na huduma za utalii wa fukwe na Visiwa "




Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati  Mhandisi Edson Ngabo amewaasa wananchi kutumia miradi ya umeme kama sehemu ya mabadiliko ya maisha  kwa kuhakikisha unatumika pia katika shughuli za kiuchumi.

 

Mhandisi Ngabo amesema Serikali inaendelea kuhakikisha miradi ya nishati jadidifu ikiwemo ya jua inakuwa na mchango mkubwa  katika gridi ya taifa na nje ya gridi huku moja ya mifano ukiwa ni mradi huo wa umeme  jua wa bei ya ruzuku uliozinduliwa pamoja na mradi wa Kishapu wa megawati 150 ambao utazinduliwa hivi karibuni. 


Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu amesema mradi wa kusambaza mifumo ya umeme jua visiwani kwa bei ya Ruzuku unatekelezwa katika mikoa minane kwa miaka miwili ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa nishati. 

 

Moja ya azimio la mpango huo ni kufikisha huduma ya umeme kwa asilimia 75 ya Watanzania  ifikapo 2030 pamoja na kuunga wateja wapya takriban milioni nane. 

 

Mhandisi Olutu amesema kuwa kwa Mkoa wa Mwanza,mradi unatekelezwa kwenye visiwa 65 kwa gharama ya shilingi bilioni 4.8  na kwamba Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 3.3 ambapo fedha iliyosalia italipwa na wananchi kupitia mfumo wa ruzuku.

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa REA, Meja jenerali mstaafu Jacobo Kingu amesema kuwa Msisitizo wa bodi hiyo ni kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora wa teknolojia na inahusisha Jamii tangu hatua za mwanzo za utekelezaji kama inavyofanyika kwenye kisiwa cha Bezi. 

 

"Wananchi wa Bezi, Mafanikio ya mradi huu hayapimwa kwa uzinduzi wake pekee, bali kwa uendelevu wake na namna mtakavyoboresha maisha yenu, Bodi itaendelea kufuatilia utekelezaji na uendeshaji wa miradi kama hii kwa kuzingatia ubora wa utekelezaji, thamani ya fedha na manufaa kwa jamii, hata hivyo uendelevu  wake utategemea ushiriki wenu katika kuzingatia matumizi sahihi ya mifumo, ulinzi wa miundombinu na ushirikiano wa watoa huduma"alisema Meja Jenerali mstaafu Kingu. 

 

Mikoa itakayonufaika na mradi wa kusambaza mifumo ya umeme jua visiwani unaolenga kuweka mifumo 20,000 ya umeme jua katika visiwa 120 ni Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Rukwa, Lindi, Mtwara na Pwani.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top