Bunge na Ipu Wasaini Mkataba Uwenyeji wa Mkutano wa 153

GEORGE MARATO TV
0


Spika wa Bunge Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) Bw. Martin Chungong leo Februari 27, 2026 wamesaini 

Mkataba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa IPU utakaofanyika Oktoba 2026 Jijini Arusha.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba huo, Mheshimiwa Zungu amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia Bunge kuwa Mwenyeji wa Mkutano huo. 



Aidha, amesema mkutano huo ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki wapatao 2,000 kutoka Mabunge wanachama 183, ni fursa adhimu kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na Tanzania kiujumla kupitia biashara za malazi, chakula, usafiri pamoja na utalii.

Spika Zungu amemhakikishia Bw. Chungong kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limejipanga vyema kuhakikisha kuwa Mkutano huo unafanyika kwa kiwango cha hali ya juu na tayari maandalizi yake yameanza kwa kuunda kamati maalum ya maandalizi inayosimamiwa na Katibu wa Bunge, Ndugu Baraka Leonard.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa IPU Bw. Chungong amesema kusainiwa kwa mkataba huu kunaonesha utayari kwa pande zote mbili yaani Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika kuandaa mkutano huo na ameishukuru Serikali kwa kukubali kuandaa mkutano wa 153 wa IPU.

Bw. Chungong amesema ana imani kuwa Mkutano huo utakaofanyika jijini Arusha utajadili mambo muhimu na kuja na suluhisho la mambo mbalimbali yanayoikumba dunia kwasasa.

Aidha, Bw. Chungong amemshukuru Rais wa IPU ambaye pia ni Spika Mstaafu, Dkt. Tulia Ackson(Mb)  kwa kujitoa kwake na kuhakikisha mkutano huu unafanyika nchini Tanzania.

Hafla ya uwekaji saini mkataba huu katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Rais wa IPU, Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mb. Naibu Spika Mhe. Daniel Sillo, Mb. Katibu wa Bunge, Ndugu Baraka Leonard, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Geneva Mhe. Balozi Dkt. Hoyce Temu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Ngwaru Magembe pamoja na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali.














Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top