Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), tarehe 16 Januari 2026,jijini Dodoma, amekutana na kufanya mazungumzo Watumishi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mkutano huo wa Dkt Rhimo Nyansaho na Wafanyakazi ulikuwa na lengo la kufahamiana na kusikiliza masuala mbalimbali yahusuyo utendaji kazi wa Wafanyakazi wa Wizara ya Ulinzi na JKT, ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na JKT, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, Wakuu wa Idara na Vitengo, Maafisa Jenerali, Maafisa wakuu, Maafisa wadogo, Askari na Watumishi wa Umma.
Katika hotuba yake kwenye kikao hicho, Waziri wa Ulinzi na JKT, alitumia fursa hiyo kuwaeleza watumishi wa Wizara ya Ulinzi na JKT Malengo na Matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Ulinzi na JKT, na akamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua ili aweze kumsaidia kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na kuendelea kupata Ustawi wa kiuchumi na maendeleo.
Dkt Rhimo Nyansaho amewahakikishia ushirikiano watumishi wa Wizara ya Ulinzi ili kuhakikisha wanatimiza na kutekeleza malengo ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Waziri wa Ulinzi na JKT, Rhimo Nyansaho amewataka watumishi kutimiza majukumu yao huku wakifahamu kuwa Serikali na wananchi wanayo imani kubwa juu yao hivyo kwa kufanya hivyo watakuwa wametimiza wajibu wao.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri wa Ulinzi azungumze, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na JKT, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, alimweleza kuwa Wizara ya Ulinzi na JKT pamoja na taasisi zilizo chini yake inaendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida na kupitia Mkutano huo na Wafanyakazi, miongozo na maelekezo yote ya Waziri wa Ulinzi na serikali yatafanyiwa kazi.
















