_Ajira mpya 12,000 za elimu na afya kuanza Januari, 2026_
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Rais wa vitendo na amethibitisha hayo katika kipindi alichoingoza Tanzania kwa kuboresha miundombinu kwenye sekta mbalimbali.
Amesema mafanikio makubwa yamepatikana chini ya uongozi wake wa miaka minne na nusu ikiwemo ujenzi wa hospitali 119 katika wilaya zisizo na hospitali, vituo vya afya 640 katika kata za kimkakati na tarafa, zahanati zaidi ya 800 vijijini pamoja na ujenzi wa shule mpya za msingi zaidi ya 2,700.
“Amejenga shule za sekondari zaidi ya 1,300 na madarasa 79,000 katika maeneo yaliyokuwa na uhitaji wa madarasa. Haya yamesaidia kuondoa tatizo la wanafunzi kusubiri kujiunga na sekondari kwa sababu ya uhaba wa madarasa. Hatua hii imemaliza utaratibu wa uchangishwaji kwa nguvu na kamatakamata za ujenzi wa vyumba vya madarasa,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Desemba 05, 2025) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa Ilemela na Nyamagana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza.
Akielezea kuhusu utendaji kazi wa Rais, Waziri Mkuu amesema ujenzi wa miundombinu bora ya elimu na afya iliyojengwa na Serikali, inahitaji watumishi wa kutosha na ndiyo maana Rais ametoa msukumo wa haraka kwenye ajira hizo na ndiyo maana aliahidi maeneo 13 ya vipaumbele ndani ya siku 100 tangu ashike madaraka.
Dkt. Mwigulu amesema ili kutekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, Serikali imeidhinisha ajira mpya 12,000 zikijumuisha 5,000 za kada ya afya na 7,000 za sekta ya elimu ambapo usaili utaanza Desemba 10, 2025 katika kila mkoa na watumishi hao wataanza kuripoti vituoni kuanzia Januari 10, 2026 hatua ambayo itaimarisha zaidi utoaji wa huduma nchini. “Nia ya Serikali ni kufanya vituo vya afya na shule zetu zipate watumishi,” amesisitiza.
Amesema kuwa Rais Samia ametekeleza mambo makubwa katika maboresho ya mifumo ya kijamii ikiwemo kuanza utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo makundi ya watoto, wazee na wajawazito ndiyo yatakuwa ya kwanza kunufaika.
Kabla ya mkutano huo, Waziri Mkuu alikagua uharibifu uliofanywa wakati wa vurugu za Oktoba 29, mwaka huu kwenye kata za Kisesa, Buzurugwa na Nyasaka ambako alioneshwa ofisi za watendaji na mali za watu binafsi zilizochomwa moto. Pia alitembelea kiwanda cha magodoro cha Banco na kuelezwa uharibifu wa mali uliofanyika.
Amewataka Watanzania wasikubali kuyumbishwa na watu wasioitakia mema Tanzania. “Kila Mtanzania anaowajibu wa kuipenda Tanzania, tusiyumbishwe na watu wasiotutakia mema, Tanzania ni ya Watanzania tuijenge na tuilinde nchi yetu. Akitokea mtu anakwambia uharibu mali ya umma, ujue huyo ana nia ya kuihujumu Tanzania, mkatalieni.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amsake mwalimu anayetuhumiwa kumbaka binti wa Mama Florah Anthony, mkazi wa Nyasaka ambaye alifikisha kilio chake mbele ya Dkt. Mwigulu.
"RPC chukua hatua, nataka nione mwisho wa suala hili. Tuma vijana wako, huyu mtuhumiwa akamatwe, uchunguzi ufanyike na ikithibitika ana hatia afunguliwe kesi ya ubakaji."
Mkuu wa Mkoa, fuatilia suala hili. Ikithibitika ametenda hilo kosa, afukuzwe kazi. Nasema afukuzwe na siyo ahamishiwe kwenye kituo kingine," amesisitiza.















