Na Mwandishi Wetu,Tanga.
Programu ya TAKUKURU Rafiki imeendelea kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi wa Mkoa wa Tanga baada ya kutatua kero 176 kati ya 248 zilizobainika katika kata 21 zilizotembelewa.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwatah, alisema kuwa programu hiyo inalenga kubaini kero zinazochochea vitendo vya rushwa katika sekta za afya, elimu, kilimo, maendeleo ya jamii, utawala na miundombinu.
“Hili ni jukwaa muhimu la kuwasikiliza wananchi moja kwa moja na kupata mrejesho wa changamoto wanazokutana nazo kwenye maeneo yao ya huduma,” alisema Ndwatah na kuongeza kuwa kazi hiyo imekuwa ikitekelezwa kwa kushirikiana na viongozi wa maeneo husika.
Kwa mujibu wa Ndwatah, kati ya kero 248 zilizopokewa, kero 72 bado zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi na TAKUKURU inashirikiana na mamlaka husika kuhakikisha zinapata majibu stahiki kwa wakati.
Aidha, alibainisha kuwa baadhi ya kero hizo zilihusiana na ucheleweshaji wa huduma, kutokuwepo kwa uwazi katika utekelezaji wa miradi, na matumizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya viongozi wa vijiji na mitaa.
“Kwa upande mwingine, programu hii imechangia pia kuwajengea uwezo watendaji wa serikali katika ngazi za msingi kuhusu namna bora ya kutoa huduma bila viashiria vya rushwa,” alieleza Ndwatah.
Aliongeza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya utekelezaji wa mikakati madhubuti ya TAKUKURU ya kuwafikia wananchi moja kwa moja na kutatua changamoto kwa wakati.
Ndwatah aliwahimiza wananchi kuendelea kutumia TAKUKURU Rafiki kama chombo cha kuwasilisha kero zao badala ya kukata tamaa au kuendekeza vitendo vya rushwa katika maisha ya kila siku.








