MwanaFA ataka wananchi wamchague tena Rais Samia*

GEORGE MARATO TV
0

 

Na Mashaka Mhando, Muheza

MGOMBEA ubunge Jimbo la Muheza  kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA, amewata wananchi wa Muheza kuendelea kukiunga mkono chama hicho kwakuwa kina dhamira ya dhati ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya wilaya hiyo iliyofanyika Septemba 10 katika Kijiji cha Bulwa tarafa ya Amani mjini hapa, MwanaFA alisema wananchi wa Muheza waendelee kukiamini chama hicho na wagombea wake kwa kuwa katika miaka mitano iliyopita wameweza kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa kiwango kikubwa.

Alisema katika miaka mitano iliyopita chama hicho kupitia serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wamefanya mambo mengi ikiwemo kupatikana kituo cha afya cha kimkakati kinachotarajiwa kujengwa katika Kijiji cha Mgambo kata ya Misalai kwenye tarafa hiyo.

Alisema tayari serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 645 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho zabuni yake imeshatangazwa kumpata mkandarasi ambaye ataanza ujenzi huo wakati wowote.

"CCM Ina dhamira ya dhati ya kutatua matatizo na changamoto zinazowakabili, naomba muendelee kumchagua Mbunge, madiwani na Rais ili tuendelee kutatua matatizo yenu," alisema.

Akielezea kwanini uzinduzi huo umefanyika tarafa ya Amani alisema ni pamoja na kuomba kura za kuwachagua wagombea wa CCM, binafsi ameutumia mkutano huo kwa ajili ya kutoa shukrani kwa namna walivyompa kura kwa asilimia 96.

"Tumekuja kuzindua kampeni Amani kwasababu siyo tu kuomba kura bali kuwashukuru kwa kunipa kura nyingi ukizijumlisha kura zote nilizopata mmenipa kura kwa asilimia 96, hili ni deni kubwa ingawa najua watu wa mlima hamyumbishwi na mambo mepesi mnaamua kwa kutumia sababu kwa yale tuliyofanya na tunayodhamiria kuyafanya, ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya katika tarafa hii," alisema.

MwanaFA alisema CCM na wagombea wake wanaomba ridhaa wachaguliwe tena kwakuwa wamefanya kazi kubwa ya kutatua changamoto hivyo kama mbunge anaomba nafasi nyingine tena ili awe mtumishi wao aendelee kufanya kazi walizokubaliana.

"Naomba endeleeni kuniamini ili niendelee kuwawakilisha niwe mtumishi wenu bahati nzuri Mimi Sina sifa mbaya kwa miaka mitano tumefanya mambo makubwa," alisema.

 Kuhusu ombi alilopewa na diwani wa kata ya Misalai kuhusu uhaba wa ardhi katika kata hiyo, alisema Rais akiwa Singida alisema serikali itawanyang'anya wawekezaji wenye mashamba ambayo hawayaendelezi licha ya makubalioano walioingia nao ya kutengeneza ajira ikiwemo uchumi jumuishi, lakini hawafanyi hivyo.

Alisema serikali imeanza kufanyia kazi na amewahakikishia wawekezaji wote wilayani Muheza, ambao wamehodhi mashamba pamoja na viwanda ambavyo hawajavifanyia kazi, watanyang'anywa na kurejeshwa kwa wananchi ili wayafanyie shughuli zao za kiuchumi.

Alisema kila jambo ambalo ni changamoto wilayani humo ameaahidi anakwenda kuyafanyia kazi kama ambavyo miaka mitano iliyokwisha amefanya na kutekelezaji miradi mingi ya maendeleo.

"Hii miaka mitano tumefanya kazi nzuri kwenye nafasi ya Ubunge, udiwani na Urais na miaka mitano hii nilikuwa najifunza ubunge ilikuwa 'Trela' na 'Movie' inakwenda kuanza," alisema MwanaFA.

Alisema hana wasiwasi na watu wa Tarafa ya Amani isipokuwa amewaomba Kila atakayekwenda kupiga kura Oktoba 29 amchukue na mwenzake ili wilaya ya Muheza iongoze kwa kumpigia kura nyingi Rais na madiwani wote wa CCM katika kata 37 zilizopo wilayani Muheza waweze kushinda, akiwemo yeye.

Alisema kimsingi wapinzani waliopo kwa Sasa wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi, wameishiwa na hawana hoja na tena wangetamani kuwa wagombea wa CCM lakini hawakuweza kutokana na ushindani uliokuwepo kwenye chama hicho.

Alisema anaowaomba wampigie kura na wagombea wenzake wa CCM kwakuwa yeye siyo mbunge mpya bali ni sheikh yule yule isipokuwa kanzu mpya kwa hiyo anayodhamira ya dhati na amedhamiria kutatua changamoto za wilaya hiyo akiwa mwakilishi wao kwakuwa miaka mitano iliyopita ameshirikiana vema na wananchi na ametekeleza miradi mingi yenye tija.

"Jamani jamani, chonde chonde angalau suala la udiwani na ubunge linaweza kuongeleka lakini suala la kumpigia kura Rais haliongeleki na halina mjadala, ndugu zangu wa Muheza nendeni mkaichague CCM na wagombea wake ili tuendelee kushirikiana kuleta maendeleo, mpeni Rais kura za kutosha wilaya yetu iweze kuongoza" alisema.

Awali diwani wa kata ya Misalai Said Mtunguja akizungumza kwa naiba ya madiwani wote walioshiriki uzinduzi huo, alisema kuwa hawana deni la mbunge Wala Rais Dkt Samia kwa namna walivyoshirikiana kutatua changamoto kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu pamoja na huduma za jamii.

"Mheshimiwa mgombea wetu hatuna deni na wewe tumeshirikiana katika miradi mingi leo hapa hakuna diwani hajapata mradi hata mfuko wa Jimbo tumeujua kupitia wewe huko nyuma hatukuwa tukiuona, tunakushukuru," alisema Mtunguja.

Diwani huyo alisema kwamba kwa Sasa tarafa hiyo changamoto pekee iliyokuwepo ni suala la wafanyakazi wa kampuni ya chai ya Usambara Mashariki (EUTCO) kukabiliwa na tatizo la kukosa mishahara kwa wakati.

Alisema wafanyakazi hao wanaweza kukaa miezi mitatu hadi minne hawalipwi mishahara yao na kufanya maisha kwa upande wao kuwa magumu ikiwemo kukabiliwa na madeni mitaani.

Pia alisema kuwa kutokana na kata hiyo kuzungukwa na mashamba makubwa ya chai, serikali ingewasaidia wananchi kupata  maeneo ambayo mwekezaji ameshindwa kuyaendeleza wapewe  wananchi wafanye Makazi pamoja na mashamba ya kulima.

Mapema mgeni rasmi katika mkutano huo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Tanga, Nassor Makau aliyemwakilisha Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah aliwataka wananchi wa Muheza kuwachagua wagombea wa CCM kwa kuwa Chama hicho kimekuja na ilani inayotekelezeka.

Alisema wananchi Wana Kila sababu ya kuwachagua wagombea wa CCM kwakuwa katika kipindi cha miaka mitano miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati imetekelezwa kwa kiwango kikubwa katika mkoa wa Tanga na Muheza kwa ujumla.

Amewaomba wananchi wampigie kura mgombea Urais wa Chama hicho Dkt Samia Suluhu Hassan, mbunge pamoja na madiwani ili waweze kushirikiana kuleta maendeleo na kamwe wasiwachague wagombea wa upinzani.

Pia katika mkutano huo aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Muheza mkwaka 2015-2020, Balozi Adad Rajab alisema Sasa ni wakati wa wananchi wa Muheza kuwa pamoja na kuvunja makundi yaliyotokana na kura za maoni na kuwa kundi moja ambalo litawachagua wagombea wa CCM kwa kishindo.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top