Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe Solomon Itunda, amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, katika hafla ya kupokea magari saba (7) aina ya Land Cruiser yaliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa Jeshi la Polisi mkoani humo.
Magari hayo yamepokelewa kama sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kipolisi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mh Itunda, amesema upatikanaji wa magari hayo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usalama na ulinzi.
Ameongeza kuwa magari hayo yataleta mapinduzi makubwa katika utendaji kazi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya.
Aidha, Mh Itunda alisisitiza kuwa serikali ya Rais Samia imekuwa ikifanya kazi kwa vitendo kwa kupeleka miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na vifaa muhimu vya kazi, ikiwemo magari hayo.
Amesema juhudi hizo zinaonesha kwa vitendo falsafa ya “kazi na utu” ambayo imekuwa dira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwatumikia Watanzania.
Mh Itunda amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa uwekezaji mkubwa wanaoufanya katika mkoa wa Mbeya akiahidi kuwa magari hayo yatatumika kikamilifu kwa malengo yaliyokusudiwa, na kuwataka askari kuhakikisha rasilimali hizo zinatunzwa kwa manufaa ya wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema magari matano kati ya hayo yatasambazwa katika Halmashauri tano za Mkoa wa Mbeya.
Amebainisha kuwa magari hayo yatakabidhiwa kwa maafisa upelelezi wa wilaya husika, ili yawe chachu ya kuongeza kasi na weledi katika kushughulikia kesi na kuhakikisha haki inapatikana kwa haraka.





