Na Mwandishi Wetu
Serikali pamoja na Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) na wadau wengine wamepongeza ubora na kiwango cha kazi za ujenzi zilizofanywa na Kampuni ya Kichina ya CRJE (Afrika Mashariki) katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Viongozi wa Mradi wa Ujuzi wa Mabadiliko na Ushirikiano wa Kikanda wa Afrika Mashariki (EASTRIP), kutoka IUCEA na Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia pamoja na Benki ya Dunia mwishoni mwa wiki, wamefanya ziara katika kampasi kuu ya Chuo hicho kwa lengo la kukagua kazi ya ujenzi katika Taasisi hiyo ina Kituo cha Umahiri katika Usafiri wa Anga.
Dk. Cosam Joseph, Mratibu wa Mradi wa EASTRIP kutoka IUCEA, alisema: "Tumeridhishwa sana na ubora wa kazi ambayo imefanywa hapa, wakandarasi wamefanya kazi kubwa wakiongozwa na uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji."
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo ya Ufundi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk.Fredrick Salukele alisema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mabweni hayo yaliyojengwa na Kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd ambapo wanafunzi wataanza kutumia hosteli hizo Novemba mwaka huu.
"Mabweni mapya mawili ya kike na kiume yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 752 kwa kila bweni. Na mwezi Novemba mabweni hayo mawili yataanza kutumika rasmi kwa wanafunzi," alisema.
Mabweni hayo mawili ni sehemu ya mradi wa majengo matano unaofadhiliwa na Benki ya Dunia chini ya EASTRIP. Mpango huu unalenga kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kuboresha malazi kwa wanafunzi.
Dk Salukele pia alisema kuwa takriban dola milioni 21 zilitengwa kutekeleza mradi wa EASTRIP katika Chuo cha NIT.
Alisisitiza kuwa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuzalisha wataalamu wa kutosha katika sekta ya uchukuzi hasa wa anga.
"Zaidi ya asilimia 80 ya dola za Kimarekani milioni 21 ziliwekwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na vifaa vya mafunzo. Leo tumetembelea maendeleo ya miundombinu, shukrani kwa timu ya usimamizi wa Chuo kwani miradi ya ujenzi imekamilika kwa asilimia 100," alisema.
Alisema ujenzi wa hangar katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwa ajili ya mafunzo ya urubani wa NIT utaanza tarehe 1 Septemba (Mwezi Ujao).
Mwisho