Na Mwandishi Wetu, Tanga
JESHI la polisi mkoani Tanga, limefanikiwa kukamata shehena ya mirungi usiku wa kuamkia jana iliyokuwa ikisafirishwa na boti na watuhumiwa kujitosa baharini kabla ya kukamatwa.
Boti hiyo aina ya fibre yenye rangi nyeupe ilikuwa Ikitokea nchi jirani ya Kenya na ilikuwa na watu wawili ambao kabla ya kutia nanga kwenye ufukwe wa kijiji cha Kwale kilichopo wilayani Mkinga, walijitosa majini kukwepa kukamatwa.
Akizungumza ofisini wake Leo Julai 22 Kamanda wa polisi mkoani Tanga Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi alisema tukio hilo limetokea alifajiri ya kuamkia leo katika kijiji hicho ambacho kipo mpakani na Jiji la Tanga eneo la Mawe mawili.
Alisema boti hiyo iliyokamatwa na askari wa kikosi cha wanamaji baada ya kupata taarifa kwamba kuna watu watapitisha mirungi kupitia bahari ya Hindi kuyaingiza Jiji Tanga.
"Tulipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kwamba kuna watu na tumia boti kuingiza mirungi katika Jiji la Tanga, tulifuatilia kwa kina na kutumia mbinu hadi tukafanikiwa kukamata hii shehena," alisema Kamanda.
ACP Mchunguzi alisema watuhumiwa wawili waliokuwa kwenye boti hiyo, walifanikiwa kutoroka baada ya kufika karibu na fukwe, lakini boti pamoja na shehena ya mirungi vilikamatwa.
Hata hivyo, Kamanda wa polisi mkoani Tanga, hakuweza kutaja uzito na idadi ya shehena hiyo iliyokamatwa.
Jiji la Tanga ni moja ya miji baadhi ya watu wake wanatumia Sana mirungi na imekuwa ikiingia kwa siri kutoka Mombasa na mingine kutoka Makanya, Same mkoani Kilimanjaro.
Hata hivyo, alisema jeshi hilo litaendelea kuimarisha doria na operesheni maalum hususan katika maeneo ya baharini ambayo yamekuwa yakitumiwa na wahalifu kuvusha bidhaa haramu kutoka nchi jirani.
Aidha, Kamanda Mchunguzi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu katika jamii, hususan vinavyohusiana na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.