📌Mitungi 16,275 kusambazwa mkoa mzima.
📌Kila wilaya kupata mitungi 3,255.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga leo Julai 11,2025 wilayani Hanang amezindua rasmi mradi wa usambazaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku mkoa wa Manyara.
uzinduzi huo umeongozwa na mkuu wa mkoa pamoja na viongozi wengine wa mkoa, wilaya, kata pamoja na vijiji na vitongoji vyake.
Mhe. Sendiga amesema lengo la uzinduzi mradi ni kuutambulisha rasmi mradi kwa wananchi wa mkoa wa Manyara ambao ndio walengwa na wanufaika wa mradi.
Mhe. Sendiga, amepongeza juhudi za Serikali na REA katika kufanikisha utekelezaji wa mradi na kuongeza kuwa lengo la Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ni kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, jambo ambalo litasaidia kutunza na kuhifadhi mazingira.
“Serikali, imeweka ruzuku ya asilimia 50, kwa hiyo wakina Baba na kina Mama wa mkoa wa Manyara, wajiandae kutumia gesi, tuwapunguzie wakina Mama kushika masizi, kutumia kuni na mikaa, kwetu sisi Mradi huu ni neema”. Alisema, Mhe. Sendiga.
Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi kutoka REA, ndugu Abdulrazack Mkomi amesema kwa nchi nzima Mradi huo wa kusambaza mitungi ya gesi ya kilo 6 kwa Wananchi utagharimu shilingi bilioni 8 ambapo kwa mkoa wa Manyara zaidi ya shilingi milioni 284 zitatumika kugharamia mitungi 16,275 kwa mkoa mzima na kila wilaya mitungi 3,255 itasambazwa
“Kampuni ya MANJIS imeshinda, tenda ya kusambaza mitungi hiyo, ilitangaza ofa ya kusambaza mtungi mmoja kwa shilingi 35,000 kwa kutambua hilo, Serikali italipia asilimia 50 ya bei hiyo, ambayo itakuwa shilingi 17,500.” Alifafanua, Mkomi.
Mkomi, amesema ili kupata mtungi huo wenye ruzuku ya Serikali kila Mwananchi anapaswa kuwa na kitambulisho cha NIDA.
Aidha Mhe. Sendiga amewaomba wananchi kutoa ushirikiano wakutosha kwa mtoa huduma (MANJIS LOGISTICS LTD) ili kufanikisha utekelezaji wa mradi na kuwasihi wananchi kutumia fursa ya upatikanaji wa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku kuweza kuachana na matumizi ya nishati zisizo salama za kupikia ili kuweza kutunza na kuboresha afya zao ,mazingira pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia.
Mkoa wa Manyara una jumla ya wilaya 5 ambazo Wananchi wake watanufaika na mitungi ya gesi ni pamoja na wilaya ya Babati, Hanang, Simanjiro, Mbulu na Kiteto.