WANAOTAKA kusafiri hadi Marekani sasa watahitajika kuwasilisha akaunti zao zote za mitandao ya kijamii kwa ukaguzi kabla ya kupewa visa na ubalozi wa nchi hiyo.
Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Marekani, kwenye taarifa, inasema wale ambao hawatawasilisha akaunti zao kwa ukaguzi, watanyimwa vyeti hivyo vya usafiri.
Japo Wizara hiyo mwezi jana ilikuwa imetangaza masharti makali ya ukaguzi wa wanaowasilisha maombi ya visa, jana ubalozi wa Marekani Nchini Kenya uliongeza hitaji lingine la ukaguzi wa akaunti za mitandao ya kijamii ya Wakenya wanaotaka visa.
“Wale wote wanaowasilisha maombi ya visa watahitajika kuwasilisha orodha ya majina au akaunti za kila mtandao wa kijamii ambao wametumia ndani ya miaka mitano iliyopita.
Orodha hiyo itawekwa katika fomu DS-160 ya maombi ya visa.
Wanaotuma maombi wanapaswa kuhakikisha kuwa maelezo yote kwenye fomu zao za maombi ya visa ni sahihi katika ya kuzitia sahihi na kutuma,” ukaeleza ubalozi wa Marekani nchini Kenya.
Hii ina maana kuwa kwa yeyote duniani wakiwemo Wakenya ambao wangetaka kusafiri hadi Marekani kauli anazoweka kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii zitatumika kubaini ikiwa anafaa kupewa visa au la.
“Ukifeli kuweka maelezo ya mitandao ya kijamii kwenye fomu yako ya maombi utanyimwa visa wakati huo na hata siku zijazo,” ikaeleza taarifa ya ubalozi wa Marekani.