MwanaFA: Rais Dkt Samia ataendelea kushirikiana na taasisi za dini

GEORGE MARATO TV
0


Na Mwandishi Wetu 

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA, amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ataendelea kushirikiana na taasisi za dini zote bila kubagua kwa ajili ya kujenga mshikamano baina ya waumini na serikali.

Akizungumza jana Juni 8 2025 katika harambee ya kuchangisha shughuli za miradi ya elimu kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki Usharika wa Muheza, alisema Rais amekuwa na upendo na taasisi za dini bila kubagua kwa kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo pale anapoalikwa na kuwaunga mkono.

"Rais wetu mmemuona juzi (wiki iliyopita) namna alivyoshiriki shughuli za kanisa akachangia kituo Cha kulelea watoto kule Bagamoyo," alisema na kuongeza,

"Amefanya hivyo kushiriki shughuli za dini kwa ajili ya kutoa haki kwa makundi yote na ameaahidi kushirikiana na dini zetu zote bila kubagua,".

MwanaFA aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha wanaliombea Taifa ili uchaguzi ufanyike kwa amani.

Alisema mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu ifikapo Oktoba mwaka huu hivyo amewataka waumini kutumia akili zao kuendeleza mshikano wa Taifa licha ya maneno mengi kusemwa ambayo msingi wake mkubwa ni kuipopoa amani iliyokuwepo.

"Najua mwaka huu ni wa uchaguzi kila neno ni neno na mambo mengi yatasemwa na yataendelea kusemwa lakini yote tuyafanye tukiwa na akili na dhamira ya mioyo yetu tukiamini maelekezo ya Mungu kwamba tuheshimu Mamlaka kwakuwa hakuna Mamlaka isiyotoka kwa Mungu, na ni muhimu kutii Mamlaka," alisema MwanaFA. 

Alisema katika kipindi Cha miaka mitano tangu mwaka 2020 hadi Sasa tunapoelekea uchaguzi mkuu serikali kupitia Rais Dkt Samia imefanya mambo mengi kutekeleza miradi ya maendeleo kwa jamii ikiwemo wilayani Muheza.

Alisema kabla ya mwaka 2020 wilaya hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo suala la ukosefu wa maji ambalo Sasa makali yake yamepungua kutokana na kutekelezwa miradi ya maji.

Alisema kata ya Kwamkabala na maeneo ya mjini Muheza, tatizo la maji lilikuwa kubwa kiasi kwamba wananchi walikuwa wakihangaika na madumu ya maji lakini Sasa baada ya kutekelezwa mradi wa maji wa shilingi bilioni 1.1 hali ya upatikanaji wa maji ni ya kuridhisha.

"Sasa hivi baada ya kuwa tumepata maji katika maeneo yetu ya mjini tatizo limebadilika wananchi wanataka kuingiza maji katika nyumba zao," alisema MwanaFA ambaye katika harambee hiyo alichangia shilingi milioni 3.

Mbunge huyo aliwatangazia waumini katika kanisa hilo kwamba atagombea tena na ubunge wake wa miaka mitano ijayo atafanya kazi hasa kwakuwa kipindi anachomaliza licha ya kufanya kazi kubwa lakini alikuwa akijifunza.

Mchungaji kiongozi wa kanisa hilo Mch Elias Majoh alisema katika harambee hiyo walikusudia kukusanya sh. 21,500,000 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kanisa ikiwemo kumalizia ujenzi wa nyumba ya watumishi ambayo tayari wameanza msingi.

Pia alisema fedha hizo zitatumika kujenga shule ya awali, msingi, sekondari na chuo katika kiwanja Chao chenye ukubwa wa ekari 25 kilichopo kata ya Genge eneo la Michungwani.

Diwani wa kata ya Majengo Mucadam Abbas na diwani wa kata ya Kwamkabala Peter Mgavilwa walimpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na mbunge huyo kwa kuleta miradi mingi ya maendeleo na waliahidi kuwaunga mkono kwa kuwachagua tena kwa kura nyingi.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top