WIZARA ya Madini,imesema itaendelea na juhudi za kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji wadogo kwa kuweka mazingira wezeshi yatakayowahamasisha kufanya uwekezaji.
Hayo yameelezwa leo Mei 2,2025 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Madini,Anthony Mavunde bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025-2026.
Waziri Mavunde amesema Serikali itaendelea kuhamasisha taasisi za kifedha kutoa mikopo ya fedha na vifaa kwa wachimbaji wadogo.
Vilevile, kuboresha utendaji wa vituo vya mfano ili kuimarisha utoaji wa huduma na mafunzo kwa wachimbaji wadogo na kuimarisha huduma za uchorongaji kwa wachimbaji wadogo.
“Wizara pia itaimarisha utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija kwa kuwatengea maeneo na kuwapatia leseni kwenye maeneo ambayo yana taarifa za jiolojia.
“Kuhamasisha wachimbaji wadogo kushiriki mikutano, maonesho na makongamano mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujifunza na kutangaza shughuli zao,”amesema Mavunde.
Mavunde amesema pia Wizara inaendelea uhamasisha wachimbaji wadogo kushiriki kwenye minada na maonesho ya madini.
Amesema katika kupambana na utoshwaji wa madini,wizara yake vyombo vingine imefanikiwa kukamata watu 75 wakitorosha madini ya aina mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 17.7.
Amesema serikali ilitaifisha madini hayo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watuhumiwa hao.
Akizungumza na George TV nje ya viwanja vya Bunge,mbunge wa Geita Vijijini mh Joseph Kasheku Msukuma,ameipongeza wizara ya madini kwa mafanikio makubwa inayoyapata.
"Kwa kweli kuna mabadiliko makubwa,kwanza kutunga kanuni za kumlinda mwekezaji na mzawa, hii ni hatua nzuri kabisa,hata kwenye makusanyo yameongezeka,lazima tumpongeze waziri na wasaidizi wake wanafanya kazi nzuri na uzalendo mkubwa"alisema Msukuma
Naye Rais wa shirikisho la wachimbaji wa madini nchini FEMATA John Wambura Bina,akizungumza nje wa viwanja vya Bunge,amesema hotuba ya bajeti iliyosomwa bungeni na waziri Mavunde imeonesha mwanga mkubwa katika sekta ya madini mchini.
"Tunampongeza sana Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan na waziri wetu wa madini,kwa kipindi kifupi cha miaka minne yamefanyika mambo makubwa hasa katika urasimishaji na kuongeze kwa uelewa kwa wachimbaji,sekta hii imeendelea kukua kila kukicha"alisema Bina
Kwa sababu hiyo ameomba wachimbaji wote wa madini nchini kuunga mkono juhudi za Rais Samia na waziri wa madini katika kuhakikisha kodi zinalipwa na kwamba shirikisho hili litaendelea kutoa ushirikiano wa mkubwa kwa seriikali katika kuhakikisha sekta ya madini inachangia kikamilifu pato la taifa.