Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amekabidhi mifuko ya Saruji ya 650 kwa ajili ya Ujenzi na ukarabati wa miradi mbalimbali jimboni kwake.
Akizungumza kwenye ziara ya makabidhiano Mjumbe wa Baraza Kuu UWT Taifa Ndg. Mariam Sagini aliyeambatana na Watumishi kutoka Ofisi ya Mbunge kwa niaba ya Mbunge amesema kuwa saruji hizo ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa ahadi zake alizoahidi katika ziara zake za kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
"Mbunge Sagini yupo kazini hachoki tayari mifuko ya Saruji inaendelea kusambazwa kwa ajili ya Ujenzi na ukarabati wa Ofisi za CCM, vyoo vya shule, Zahanati na taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini hiki ni kiashiria tosha kuwa mbunge amekuwa wa vitendo na mtekelezaji pia anatosha kuwakilisha wananchi wa Jimbo la Butiama," amesema Mariam Sagini.
Naye Afisa Mahusiano kutoka Ofisi ya Mbunge Ndg. Japhet Changarawe amewaomba wananchi kushirikiana na wana-CCM wengine kumpa ushirikiano mbunge Sagini ili aendelee na majukumu yake ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 - 2025.
Changarawe ametaja Kata ambazo zimekabidhiwa Saruji kwa awamu ya kwanza kuwa ni Buruma, Butuguri, Butiama, Kyanyari, Bwiregi, Nyamimange, Sirorisimba, Buswahili, Nyankanga na Bisumwa.
Baadhi ya wanufaika wa saruji hizo wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi na kusema kwamba wamepunguziwa gharama za ujenzi na ukarabati kwenye miradi husika.



