📍 Awataka kutumia malengo matatu ya Jumuiya hiyo, kuipa ushindi CCM 2025
📍 Awataka wawe mfano bora kwa jumuiya nyingine, kwakutokua sehemu ya makundi
📍 Aeleza mmomonyoko wa maadili, kasi ya Vijana kuuza mihadarati, usagaji na ushoga
📍 Aitaka Jumuiya kushirikiana na Wazazi kukomesha hali hiyo
📍 Mwenyekiti wa Wazazi ataka wamchague mbunge kwa faida ya wilaya badala ya Matumbo yao.
📍 Katibu Siza aahidi ushindi mkubwa kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
Na Mwandishi Wetu, Mkinga
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Gilbert Kailima ambaye kwa Sasa ni Mkuu wa wilaya ya Mkinga, amewapiga msasa viongozi na wajumbe wa jumuiya hiyo wilayani hapa kuelekea uchaguzi Mkuu ujao.
Akizungumza katika Kongamano la Elimu na Malezi lililoandaliwa na Jumuiya hiyo wilayani hapa, April 6 2025, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka Wazazi kuzingatia dhima na malengo ya kuanzishwa Jumuiya hiyo mwaka 1955, kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa faida ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aliwakumbusha misingi na malengo ya Jumuiya hiyo kuwa ni Elimu, Malezi na Mazingira ambapo watakapotekeleza majukumu hayo watakirahisishia ushindi chama kwa kufuatilia utekelezaji wa ilani.
Alisema kuwa katika elimu jumuiya hiyo ikutane na Kamati za shule, walimu lakini pia kufahamu changamoto zilizoainishwa kwenye ilani ya CCM na kuyajadili kwenye vikao na kuyatafutia majawabu katika ngazi husika.
Alisema Jumuiya hiyo iyasemee mambo mazuri yaliyotekelezwa na serikali ili wananchi wayajue kwakuwa serikali imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu, afya, barabara, Umeme, maji na miundombinu.
Alisema serikali imeleta jumla ya shilingi bilioni 1.3 kwa ajili maendeleo ikiwemo kujenga hospitali ya wilaya, pia ikaleta shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Cha ufundi stadi (VETTA) kilichoanza kufundisha wanafunzi mwaka huu.
Hata hivyo, alisikitika ofa iliyotolewa na Mbunge wa Mkinga na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dastan Kitandula ya kusomesha watoto 50 katika Chuo hicho, lakini hadi sasa hakuna mzazi aliyechangamkia ofa hiyo.
Katika suala la malezi Mkuu wa wilaya alisikitika kujitokeza wimbi la Vijana wanaojihusisha na uuzaji wa mihadarati ikiwemo kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Alisema hivi karibuni katika kata ya Moa mtoto mmoja wa shule mwenye umri wa miaka 11 alikamatwa akiuza Mirungi shuleni kwa wanafunzi wenzake akida ametumwa na mzazi wake.
"Tumemkamata mtoto wa miaka 11 akiwauzia wenzake Mirungi, kile kichungi aliuza sh 100 na alisema ametumwa na mama yake, akiuza akirudi na pesa wananunua samaki," alisema.
Akionesha ukubwa wa tatizo hilo, Mkuu wa wilaya alisema mwaka jana vijana 15 kati ya 36 waliokuwa wamejiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutoka wilayani humo, walirudishwa nyumbani baada ya kubainika wakijihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Pia Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mkinga Amani Kasinya akitoa salamu kwenye kongamano hilo, aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kurejea katika Utamaduni wa wilaya na kuachana na vitendo vya ushoga na usagaji.
Mwenyekiti wa Umoja wa vijana UVCCM wilayani Mkinga, Aisha Rashid akitoa salamu kwenye baraza hilo alisema kuwa vijana wa wilaya hiyo wapo tayari kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi CCM kinashinda katika nafasi ya udiwani, ubunge na Urais.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya Wazazi Ramadhani Nyuni aliwataka Wazazi kuhakikisha wakati ukifika wawachague wagombea watakaokuwa na maslahi na wilaya hiyo ili iweze kupiga hatua na kamwe wasichague wagombea kwa ajili ya maslahi yao.
Katibu wa Wazazi wa wilaya hiyo Siza Mhegele Alisema kongamano hilo limefanyika ikiwa ni wiki ya wazazi na kwamba tayari wameanza kwa kupanda miti pamoja na kufanya usafi lakini pia tayari wameunda Kamati za ushindi kwa ajili ya uchaguzi Mkuu ujao.
Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa na mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wazazi wilayani Mkinga Harith Bakari, amewataka wazazi wilayani hapa, kushirikiana na viongozi ili kuhakikisha mmomonyoko wa maadili kwa vijana unadhibitiwa ikiwemo kuacha kuwapenda watoto kupitiliza.

.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)