Na Mashaka Mhando, Muheza
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amezindua mashindano ya mbio za magari maarufu kama Dar TT Drag Race katika eneo la Kigombe, Wilaya ya Muheza.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mashindano hayo, Balozi Dkt. Batilda ameipongeza timu ya Dar TT kwa kuichagua Tanga kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, akisema kuwa hatua hiyo itafungua fursa za kiuchumi kupitia sekta ya michezo.
Balozi Dkt. Batilda amewakaribisha waratibu na wanamichezo wa mashindano ya aina hiyo kuendelea kuitumia barabara ya Tanga–Pangani kwa shughuli zao, akibainisha kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa barabara hiyo kama sehemu ya kukuza uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Tanga
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainabu Abdallah, amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kujitoa na kushirikiana kikamilifu katika kuendeleza michezo, hatua ambayo inaonesha dhamira ya dhati ya kumuunga mkono Rais Dkt. Samia katika maendeleo ya sekta ya michezo nchini.
Naye Mratibu wa Dar TT, Ally Mchahaga, ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Tanga kwa kuwapa ushirikiano mkubwa, na kuahidi kuendelea kuichagua Tanga kama sehemu ya mashindano yajayo kutokana na mwitikio mzuri walioupata.
Mwisho