GHATI MSAMBA ,Serengeti
Taasisi ya Nyansaho Foundation, yenye makao makuu Wilayani Serengeti, imeshiriki kikamilifu katika mapokezi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, aliyefika wilayani humo kwa ziara maalum ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 - 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa taasisi hiyo Aprili 26, 2025, Mjumbe mwakilishi wa Nyansaho Foundation, Mtiro Gekora Kitigani, alieleza kuwa wao wameupokea ugeni huo kwa mikono miwili na ni fahari kubwa kwa wananchi wa Serengeti.
"Sisi kama Nyansaho Foundation tumeupokea ujio wa Dk. Nchimbi kwa mikono miwili, na ni fahari kubwa kwa wananchi wa Serengeti. Tunamshukuru Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara pamoja na Mkuu wa Mkoa kwa kutambua uwepo wetu na juhudi zetu ambazo zinaonekana hapa Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla," alisema Kitigani.
Aliongeza kuwa taasisi yao imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia sekta ya elimu, afya, pamoja na kusaidia watu wenye mahitaji maalum ndani na nje ya Wilaya ya Serengeti.
"Taasisi hii inajishughulisha na kusapoti masuala ya elimu, afya, pamoja na kuwasaidia watu wasiojiweza, siyo tu ndani ya Serengeti bali pia katika maeneo mengine nchini," alisema.
Aidha, Kitigani aliweka bayana kuwa taasisi yao itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali.
"Tunamuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wasaidizi wake. Sisi tupo nyuma yao, tukisapoti na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo, hususan kwenye sekta ya afya, elimu na mahitaji maalum kwa wasiojiweza," alifafanua.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi, aliwataka wananchi wa Wilaya ya Serengeti kudumisha Muungano wa Tanzania kwa kujenga mshikamano, amani, na upendo, ili kuwaenzi waasisi wa taifa akiwemo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
"Ni wajibu wetu kama Watanzania kuendeleza Muungano wetu kwa kujenga mshikamano, kuimarisha amani na kudumisha upendo miongoni mwetu. Huo ndiyo msingi wa maendeleo endelevu ya taifa letu," alisema Dk. Nchimbi.
Katika ziara hiyo, Dk. Nchimbi pia alielezea furaha yake kwa mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka kwa wananchi wa Serengeti.
"Nawashukuru wananchi wa Serengeti kwa mapokezi makubwa, yenye bashasha, upendo na hamasa kubwa. Mapokezi yenu ni ishara ya mshikamano na mapenzi yenu kwa Chama chetu na taifa kwa ujumla," alisema.
Dk. Nchimbi alisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Ilani yake, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na serikali na viongozi wao katika kuleta maendeleo.
Mwisho.