Mzee Butiku atoa haya kwa Rais Samia

GEORGE MARATO TV
0


-Ampa asilimia 85 kiutendaji

-Ashangaa wanazungumzia ukubwa wa deni la taifa bila kujivunia miradi iliyopo

-Atoa heko kwa CCM  kumteua kuwa mgombea wake 

-Awaonya Chadema,asema hakuna mwenye mamlaka kuzuia uchaguzi


Na George Marato-gmtv

Mwenyekiti wa taasisi ya Mwalimu Nyerere mzee Joseph Butiku,amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo,ikiwemo inayolenga kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Mzee Butiku ameyasema hayo ofisini kwake jijini  Dar es Salaam katika mahojiano maalum,ambapo amesema kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi hiyo hasa ya sekta ya nishati,maji,elimu,afya,Reli na barabara katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia imewaziba midomo baadhi ya watu.

Amesema kuwa hakuna ubishi kuwa Rais Samia ameonesha utashi na mapenzi makubwa kwa taifa lake hasa katika kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo wa Reli,Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere na ujenzi wa madaraja makubwa likiwemo la Busisi.



Amesema mbali na kutekeleza miradi hiyo mikubwa,serikali ya awamu imesimamia vema katika suala la haki na usawa kwa kila mtanzania na kutoa uhuru wa watu kujieleza na kwamba,bado kuna tatizo kwenye eneo la maadili ambalo pia linahitaji nguvu ya pamoja kati ya serikali na wananchi.

"Hili la maadili hatuwezi kumtwisha mzigo Rais wetu,hili letu,wewe ni baba au mama una wajibu wa kutoa maelezi katika familia yako,tukifanya hivi hata vitendo vya rushwa vitakwisha,....mtoto anatoka chuo kikuu ananza kazi tu ananunua gari ya kifahari na kujenga nyumba nzuri,wewe mzazi unashangilia badala kumuuliza pesa hizo kwa mwaka mmoja tu amezitoa wapi kama sio mwizi" alisema mzee Butiku

Kwa sababu hiyo mzee Butiku amewaomba watanzania kuendelea kumpa ushirikiano  Rais Samia na serikali yake ili iweze kutimiza wajibu wake wa kuwaletea wananchi maendeleo wanayokusudia.

"Mimi si mtu wa kusifia sifia viongozi hasa Rais kwani ni wajibu wake kufanya hivyo,lakini kwa kazi hii kubwa anayoifanya Rais wetu(Samia) katika usimamizi na ujenzi wa miradi hii mikubwa nasema wazi kabisa nampongeza sana,amefanya kazi kubwa kwa taifa letu"alisema Butiku na kuongeza.

"Zamani kwenye uongozi tulikuwa tunatoa maksi(alama) si hizi zenu za siku hizi,kwa sababu hii na kuridhishwa kwangu na kazi anazofanya Rais wangu, nampa alama 85,nasema wazi kibisa,nampa 85 anastahili kabisa na hizo kumi na tano zilizobaki ni zetu nasi tufanye kumsaidia Rais"alisema.

Kuhusu kukuwa kwa deni la   taifa,mzee Butiku amesema hawezi kushangaa kuongezeka kwa deni hilo kutokana na miradi mikubwa iliyojengwa nchini.

Alisema miradi mingi ilihitaji fedha nyingi ili iweze kukamilika na si kosa kwa serikali kukopa na kujenga miradi kama hiyo ya reli,bwawa la mwalimu Nyerere na madaraja makubwa ambayo yataleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi.



"Kosa ambalo serikali inafanya haitaki kuwaambia wananchi kuwa deni hili linatokana na hiki na hiki,serikali imefanya mambo makubwa sasa lazima ikope ili kutekeleza hayo na lazima serikali itoe elimu kwa wananchi wajue fedha hizo hazijakopwa na Samia (Rais)kwenda kujenga nyumba yake,zimekopwa na serikali zimeingia kwenye miradi ikiwemo ya treni hii tunayofurahia ndio matunda yake"alisema mzee Butiku

Hata hivyo mzee Butiku alishauri serikali  kuharakikusha miradi ya makaa ya mawe na ule wa chuma cha Liganga ambayo amesema inaweza kulisaidia sehemu kubwa taifa hili.


"Pamoja na miradi hiyo ambayo ingeweza kutuingizia fedha za kigeni lakini pia tuna wajibu kama Watanzania kufufua viwanda vya nguo,tulime mazao kwa wingi yakiwemo ya Pamba,katani  mbaazi na mengine,haya yanaweza kutuingizia fedha nyingi za kigeni na hivyo kuiuza uchumi wetu.




Katika mahojiano hayo mzee Butiku ambaye pia ni kada mtiifu wa chama cha mapinduzi CCM,ametoa maoni yake kuhusu kuteuliwa kwa Rais Samia kugombea Urais kupitia chama  hicho amesema jambo hilo limefanyika kwa wakati mwafaka na kupongeza uamzi wa mkutano mkuu wa CCM.

"CCM  ina taratibu zake za kumpata mgombea wake  wa Urais,siku ile mimi nilipewa mwaliko bahati mbaya sikuwa sawa kiafya hivyo sikwenda Dodoma lakini niliona kwenye runinga,mambo yote yalikuwa wazi,hoja ilipotolewa,viongozi hawakuiubali pale walijua wangekiuka taratibu,walihairisha mkutano ule kwa muda wakaenda kufuata taratibu na baada ya hapo uamuzi  ukafanyika hivyo ccm haijakosea hata kidogo kwa  jambo hilo"alisema Butiku.

Mzee Butiku ametumia mahojiano hayo pia kuonya kikundi au watu wenye nia ovu kutaka kuzuia uchaguzi mkuu wa madiwani,wabenge na Rais huku akisema hakuna mwenye mamlaka wa kufanya hivyo.

Amesema kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imatoa nafasi kila baada ya miaka mitano wananchi wanapata haki ya kuchaguzi viongozi wao,hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuwapora haki hiyo wananchi.

"Nimesikia mara No reform no Election,hii haikubaki hata kidogo,hakuna mwenye mamlaka ya kuzuia uchaguzi,kama wanadhani kuna mifumo haipo sawa wakae wazungunze na kama jambo ni kubwa baada ya uchaguzi jambo hilo lirekebishwe kakini kamwe hakuna mtu au taasisi ya kuzuia uchaguzi huu sasa"akisema mzee Butiku.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top